SUAMEDIA

Wazazi wahimizwa kushiriki malezi ya awali ili kukuza afya na akili za watoto

 Na: Farida Mkongwe

Wazazi na walezi wametakiwa kuwekeza muda wa kuwa karibu na watoto wao katika hatua ya makuzi ya awali, kwani hatua hiyo ndiyo msingi wa kuunda kizazi chenye afya bora, maadili mema, na uwezo mpana wa kufikiri.

Hayo yameelezwa na Fredrick Joseph Kilawe, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Lishe ya Binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakati akizungumza katika banda la Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Mlaji kwenye maonesho ya kilimo Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mkoani Morogoro.

Kilawe amesema kipindi cha makuzi ya awali, kuanzia umri wa miaka miwili hadi minane, ni muhimu sana kwa ukuaji wa akili ya mtoto, ambapo ubongo wake hukua kwa kasi na uwezo wa kujifunza huimarika kwa kiwango kikubwa hivyo kuwataka wazazi kushirikina na watoto wao katika michezo, mazungumzo, na kazi ndogo ndogo za ubunifu ambazo huchangia katika ukuaji wa mtoto kihisia na kiakili.

Ameeleza wamebuni mbinu rahisi za malezi kupitia vifaa vya kujifunzia vinavyotumia malighafi zinazopatikana majumbani kama vile maboksi, karatasi na plastiki za kurejelewa ili kutengeneza picha, midoli, mipira na vifaa vingine vya kufundishia watoto masomo kama hesabu, lugha na maumbo.

“Mbinu hizi si tu kwamba zinamsaidia mtoto kuwa mwepesi wa kujifunza, bali pia zinajenga ukaribu kati ya mzazi na mtoto, kukuza maadili, ubunifu na uwezo wa kushirikiana na watu wengine,” amesema.

Amesema kutokana na maendeleo ya teknolojia, watoto wengi hutumia muda mwingi kwenye simu na vifaa vya kidijitali, hali ambayo hupunguza mwingiliano wa kijamii na kuathiri makuzi yao na kwamba, elimu kwa wazazi na walimu juu ya jinsi ya kuandaa michezo ya kujifunza ni muhimu sana.

"Ushauri wangu kwa wazazi ni kujifunza kutengeneza vifaa vya kuchezea na kufundishia watoto wao kwa kutumia malighafi rahisi zinazopatikana majumbani, pia washiriki moja kwa moja na watoto wao katika shughuli hizi ili kujenga mahusiano ya karibu, kukuza maadili, na kusaidia makuzi ya kijamii na kiakili ya watoto wao," amesema Kilawe.

 

Post a Comment

0 Comments