Na: Hadija Zahoro
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetangazwa kuwa Makao Makuu ya Jukwaa la Kimataifa
linalolenga kuimarisha ubadilishanaji wa maarifa, teknolojia na biashara katika
sekta ya kilimo na biashara Afrika (CEBOT), kutokana na mchango wake mkubwa
katika tafiti za kilimo, ubunifu wa teknolojia, na maendeleo ya mifumo endelevu
ya uzalishaji wa chakula.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kukuza ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya kilimo na biashara kwa kutumia rasilimali na tafiti zinazofanyika barani Afrika, hususan kupitia taasisi zinazotambulika kitaaluma kama SUA.
Akizungumza katika hafla
maalum ya uzinduzi iliyofanyika SUA ikihusisha Menejiment ya Chuo hicho,
Mkurugenzi wa Taasisi ya CEBOT na wawakilishi wake, Mkurugenzi Msaidizi wa
Masuala ya Utawala na Maendeleo ya Biashara Barani Afrika, Denice Christian,
ameeleza kuwa uteuzi wa SUA umetokana na ukubwa wa Chuo hicho kitaaluma, pamoja
na mchango wake katika masuala mtambuka ya kilimo, mazingira, ujasiriamali na
ubunifu mbalimbali.
‘‘Kama mnavyojua kwa sasa hakuna misaada (USAID),sasa hivi tunaingia
kwenye utawala wa kibiashara ndiyo maana tukasema kwamba tuanzishe ofisi SUA
kwani ni Chuo ambacho kina wanafunzi wengi na kitaweza kuunganisha vyuo vyote
vya kilimo ukanda wa Afrika’’ ameongeza Denice.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam SUA, Prof. Japhet Kashaigili, ameeleza kuwa hatua hiyo inawapa fursa ya kutekeleza makubaliano ya ushirikiano kwa kushirikiana katika teknolojia mbalimbali zinazohusu mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, ikiwemo uzalishaji wa mazao shambani pamoja na mifugo.
Kwa sasa SUA tayari imeanzisha miradi kadhaa inayolenga kuongeza tija ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia na ubunifu, hatua inayotajwa kuwa msingi wa mafanikio ya CEBOT katika kipindi cha miaka mitano ya ushirikiano huo (2025–2030).
0 Comments