SUAMEDIA

Elimu ya Amali yaanza kutoa matunda SUA kupitia sekondari ya Mafiga

 Na: Josephine Mallango 

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimepokea kwa vitendo Sera mpya ya Serikali ya Elimu ya Mkondo mpya wa Amali ya mwaka 2023, ambapo tayari wanafunzi wa shule ya sekondari Mafiga waliopo chini ya SUA wamezalisha kwa vitendo bustani za mfano za mbinu shirikishi za kilimo cha mjini, hali ambayo imeongeza muamko mkubwa wa wazazi kufurahia watoto wao kujifunza elimu ya amali, huku idadi ya wanafunzi ikiongezeka kutoka 58 walioanza hadi kufikia 218.

Dkt. Hamidu Khalfan, Mtafiti na Msimamizi wa Elimu ya Amali kutoka Shule Kuu ya Amali SUA, amesema sera hiyo mpya ya elimu ilianzishwa mwaka 2023 ambapo SUA walianza na wanafunzi 58 kutoka sekondari ya Mafiga na sasa wamefikia wanafunzi 218 ambapo mpango wa muda mrefu wa SUA ni kuhakikisha zaidi ya wanafunzi 5,000 wa sekondari watakuwa wamenufaika na elimu ya amali kila mwaka kwa ngazi ya kidato cha nne na cha sita.

Amesema sera hiyo ya Elimu ya Amali ililenga kubadilisha mfumo wa elimu wa zamani, ambapo badala ya wanafunzi kujifunza taaluma ya jumla, sasa wanajifunza mikondo mbalimbali ya amali inayowawezesha kupata ujuzi wa fani wanazopenda kupitia mafunzo ya vitendo.

Dkt. Khalfan ameongeza kuwa tayari SUA ina mikondo mitatu ya elimu ya amali ambayo ni Elimu ya Mazao kupitia vibanda, ambapo wanafunzi wa Sekondari ya Mafiga wamejikita, mkondo wa pili ni elimu ya vitalu vya mimea, bustani za mazao ya chakula, maua na bustani za mazao mbalimbali na mkondo wa tatu unahusu ufugaji wa wanyama kwa kuzingatia mbinu bora za ufugaji, afya za mifugo na njia sahihi za kupata mazao bora na ya kisasa.

Ameeleza kuwa Shule Kuu ya Elimu SUA imepewa jukumu la kulea Shule ya Sekondari ya Mafiga, ambapo wanafunzi wameanza kufundishwa kwa vitendo kuhusu sayansi ya kilimo cha mboga na kilimo cha mjini mafunzo yanayojumuisha hatua zote kutoka kupanda miche, kukuza mimea hadi kuvuna, pamoja na mafunzo ya umwagiliaji wa matone (drip irrigation), uvunaji na uhifadhi wa maji.

Dkt. Khalfan amesema SUA kwa sasa imeanzisha shahada sita za Elimu ya Amali kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita kuendeleza ujuzi walioupata.

Kupitia shahada hizo, wanafunzi wanaweza kujiunga na SUA na hatimaye kuwa walimu wa elimu ya amali mashuleni ambapo walimu wa elimu hiyo wanatakiwa kuwa na zana shirikishi na vifaa vya kufundishia vinavyojieleza vyenyewe kwa ufasaha.

Ameongeza kuwa kwa sasa wanafunzi waliopo ni 218, lakini bado shule ina nafasi ya kupokea wanafunzi wengi zaidi kwa kuwa SUA iko tayari kumuunga mkono Rais Dkt.Samia katika kuhakikisha kuwa mipango ya Serikali inatekelezwa kwa vitendo kupitia taasisi zake, lengo kuu likiwa ni kuhakikisha vijana wanajengewa uwezo wa kujiajiri kupitia elimu ya amali baada ya kumaliza kidato cha nne au sita.






 

Post a Comment

0 Comments