Na: Siwema Malibiche
Wakulima
nchini wametakiwa kutumia teknolojia za kilimo ipasavyo katika kukuza sekta ya
kilimo ili kuongeza uzalishaji kwa kuachana na kilimo cha mazoea, ili Taifa
liweze kupata maendeleo.
Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Julius Nyerere, Nanenane 2025, mkoani Morogoro, ambapo amebainisha kuwa sekta ya kilimo ina fursa lukuki ambazo iwapo zitatumika kikamilifu kwa kutumia zana za kisasa, Tanzania itapiga hatua kubwa kimaendeleo.
Waziri Mkuu huyo Mstaafu ameitaka jamii
kuyatumia maonesho hayo ya wakulima kama darasa la kujifunza na kujiongezea
maarifa, ujuzi na weledi kutoka kwa wataalamu mbalimbali walioko katika mabanda
tofauti, ikiwemo banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Vile vile, amesisitiza ushirikiano na mshikamano
baina ya taasisi za umma na binafsi katika kuendeleza uwekezaji nchini ili
kuongeza na kuboresha mnyororo wa thamani katika sekta ya ufugaji, uvuvi na
kilimo cha mazao nchini, huku wakiendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya chakula
lishe.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo Mstaafu amewataka wananchi kujitokeza
na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kutumia haki
yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wao watakaoleta maendeleo katika maeneo
yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, amesema kuwa Kanda ya Mashariki inajivunia kuwa miongoni mwa maonesho bora nchini kwa kushirikisha jamii ipasavyo, na kama uongozi itaendelea kuboresha kadri miaka inavyokwenda ili kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo.
Maonesho hayo ya wakulima Kanda ya Mashariki
yamehusisha mikoa minne ambayo ni Morogoro, Pwani, Tanga na Dar es Salaam,
yaliyoongozwa na kauli mbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
2025.”
0 Comments