SUAMEDIA

Popo wasaidia kuhifadhi mazingira na kupambana na malaria - Utafiti SUA

 

Na: Josephine Mallango

Wananchi wameshauriwa wasiharibu mapango ya popo katika ekolojia kwa kuwa ni muhimu, kutokana na ukweli kwamba popo hutumika kusambaza mbegu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hutengeneza misitu, huondoa wadudu waharibifu kutoka mashambani na hupunguza maambukizi ya malaria na chikungunya huku mbolea ya popo ikitajwa kuwa na virutubisho vingi kuliko mbolea nyingine.


Hayo yamesemwa na Dkt. Edson Kinimi, Mratibu wa Maabara inayotembea kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambapo amesema kuwa popo katika ekolojia pia hutumika sana kuchavusha mimea, ikiwemo maua, kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Amesema popo huondoa wadudu waharibifu mashambani kwa kuwala, ambapo popo mmoja mdogo anakula mdudu wa saizi ya mbu zaidi ya 5,000 kwa siku hivyo kusaidia kupunguza malaria na magonjwa mengine yanayotokana na mbu kama chikungunya na unyongi-nyongi, kwa kutumiwa katika ekolojia.

Mratibu huyo wa Maabara Inayotembea ameongeza kuwa wamebaini kuwa katika maeneo ya ekolojia kuna watu wanaoshambulia popo na kuwaua ili waondoke kwenye mapango, ili wachimbe madini hali ambayo inaweza kuhatarisha ustawi wa ekolojia ya Mto Kagera na kuleta madhara ikiwemo kupotea kwa misitu, miti ya dawa, rasilimali ya matunda na mbao za thamani kubwa ndiyo maana wameandika makala ya kisayansi wanayotarajia kuchapishwa kwenye majarida makubwa ya kisayansi ili kusaidia kuhifadhi mapango hayo ya popo.

Dkt. Kinimi amesema hayo wakati akielezea utafiti wa ugonjwa wa Marburg ambao kwa sasa umedhibitiwa nchini, lakini watafiti bado wanaendelea kuchukua vinasaba vya popo wa Tanzania walioko kwenye Mto Kagera, ili kubaini endapo popo hao wana vimelea vya ugonjwa huo au kama ugonjwa huo umetoka nje ya Tanzania akisema kuwa wamegundua mapango matano yenye popo takriban laki moja katika kila pango kwenye ekolojia ya Mto Kagera.

"Kuna popo zaidi ya aina 400, sisi tunafanya utafiti na popo aina ya Egyptian fruit bats (popo wanaokula matunda), tunachukua sampuli kutoka kwa popo wetu na kuendelea na utafiti, ambapo kwa sasa tunapeleka sampuli kwenye vipimo vikubwa zaidi vya vinasaba ili kuona kama vina vimelea vya Marburg au vimelea vingine, hivyo kwa sasa hatuwezi kusema chochote hadi tumalize majaribio tunayoendelea nayo katika utafiti huu," amesema Dkt. Kinimi.

Akizungumzia kuhusu sababu ya kulipuka kwa ugonjwa wa Marburg mwaka huu 2025, tofauti na miaka ya nyuma, amesema hali hiyo imesababishwa na ongezeko la watu duniani, ambalo limepelekea binadamu kusongelea maeneo ya mapori ambayo ni makazi ya wanyama, hali hiyo inaongeza mwingiliano kati ya binadamu na wanyama, ambapo baadhi ya watu hutafuta chakula, na wengine hutumia popo kama chanzo cha protini.

"Kuna watu wanatumia popo kama chanzo cha protini, hasa kwenye maeneo ya machimbo ya madini ya bati kule Kagera, wakati wa utafiti, tumekuta kuna mwingiliano wa makabila mbalimbali kutoka Afrika Mashariki na mataifa mengine yanayotumia popo kama chakula, ikiwemo Wachina, hali hiyo inawashawishi Watanzania wengine kujifunza na kutamani kuonja," amesema Dkt. Kinimi.

Wakati mwingine popo hula matunda na kuyaangusha, watu huchukua na kula matunda hayo, na hata tumbili na nyani huchukua na kula matunda yaliyong’atwa na popo, jambo ambalo ni mojawapo ya njia ya maambukizi ya ugonjwa wa Marburg.

Mratibu huyo wa Maabara Inayotembea amesema popo wanatoa mbolea ambayo imethibitika kuwa bora zaidi na ina virutubisho vya kutosha kuliko mbolea nyingine ambapo watu hutumia mbolea hiyo kustawisha mazao kama nyanya na mahindi kwa hiyo wanaingia kwenye mapango bila vifaa vya kujilinda wala tahadhari yoyote.

Amesema kutokana na umuhimu wa popo katika ekolojia,  wakati wa kutoa majibu ya utafiti, watawashirikisha viongozi wa Mkoa wa Kagera ili kutoa elimu ya kuishi na popo kwa manufaa ya ekolojia.

 

Post a Comment

0 Comments