Na: Josephine
Mallango
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Idara ya Sayansi ya Udongo na Jiolojia
kimesisitiza kuwa ni muhimu kwa mkulima anayelenga kulima kwa tija kuhakikisha
anapima afya ya udongo pamoja na afya ya mbegu atakazozitumia kabla ya kuanza
shughuli za kilimo, ili kuepuka hasara na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Dkt. Hellen Kayagha kutoka SUA amesema katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea, Chuo hicho kinatoa huduma ya bure ya upimaji wa afya ya udongo, mimea na mbegu.
Amesema
huduma hiyo inatolewa kwa wakulima na wageni mbalimbali wanaotembelea banda la
SUA, ambapo sampuli zinapokelewa na majibu hutolewa ndani ya saa moja tu, hapo
hapo bandani.
“Kwanini
ni muhimu mkulima kupima udongo, kwa sababu inamsaidia kufahamu kiasi cha
virutubisho kilichopo katika udongo na inampa uwezo wa kujua aina ya mbolea
anayotakiwa kutumia na aina gani ya virutubisho ambavyo vinatakiwa kuongezwa
kwenye udongo wake ili aweze kulima kwa tija na kupata mazao bora na yenye afya
bora,” amesema Dkt. Kayagha.
Kwa upande wa mbegu, amesema mkulima anapoangalia afya ya mbegu anazotumia atakuwa na uhakika wa mbegu anayopanda inaota kwa kiasi gani shambani.
Ameongeza
kuwa SUA wanafundisha njia rahisi za kufanya majaribio ya uotaji wa mbegu kabla
ya kupeleka shambani, jambo litakalomsaidia mkulima kuepuka hasara za kupanda
na kurudia tena badala yake, atapanda mbegu akiwa na uhakika kuwa ikipandwa
itaota shambani.
Dkt.
Kayagha amebainisha kuwa pamoja na kwamba wanapatikana Nanenane kwa sasa kwenye
mabanda ya maonyesho wakiwa na vifaa vya kisasa ikiwemo maabara ya udongo
inayojibika (mobile soil laboratory testing kit) yenye uwezo wa kupima
virutubisho vinavyopatikana kwenye udongo ikiwemo tindikali, huduma hizo
zinaendelea kupatikana chuoni ambako kuna vifaa vya kisasa na gharama za
upimaji ni nafuu kabisa ambazo mkulima yoyote anaweza kumudu.



0 Comments