Na: Siwema Malibiche
Wakulima wametakiwa
kutumia Ghala la Mkulima kutoka Maktaba ya Taifa ya Kilimo iliyopo katika Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupata maarifa, ujuzi na teknolojia
mbalimbali za kilimo ili kuongeza tija na faida katika uzalishaji wa mazao.
Wito huo umetolewa na Mkutubi na Msimamizi kutoka Idara ya Rejea na Huduma kwa Jamii wa Maktaba hiyo, Bw. Jabir Jabir, katika maonesho ya wakulima yanayoendelea Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, ambapo amesema kilimo bora ni kile kinachofanyika kwa kufuata taarifa na maarifa sahihi kutoka kwa wataalamu.
Ameeleza
kuwa licha ya kuwepo kwa vitabu vingi ambavyo wakulima wanaweza kuvisoma, pia
wanaweza kujifunza kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu janja kupitia
"Mkulima Collection", ambapo hupata mafunzo mbalimbali kutoka kwa
wataalamu waliobobea katika sekta ya kilimo.
Amesema maktaba hiyo
inakawaribisha watu wa kada zote kupata maarifa bila kujali kiwango cha elimu,
na kusisitiza kuwa katika kitengo cha Ghala la Mkulima wanakusanya taarifa na
machapisho mbalimbali yanayotokana na tafiti zilizofanywa na SUA pamoja na
watafiti wengine kutoka taasisi mbalimbali, yaliyoandikwa kwa lugha rahisi
inayomuwezesha mkulima kuelewa kwa urahisi.
Vile vile, ameitaka jamii kujikita zaidi katika kutafuta maarifa ya kilimo kabla ya kuanza shughuli za kilimo ili kufanikisha uzalishaji wenye tija. Amesisitiza kuwa SUA ina machapisho mengi ambayo yanaweza kumsaidia mkulima kujisomea akiwa mahali popote duniani.
Maktaba ya Taifa ya Kilimo iliyopo SUA
Kampasi ya Edward Moringe inalenga kusaidia wakulima kupata taarifa muhimu kuhusu
kilimo, mifugo na uvuvi ambapo kupitia machapisho mbalimbali, wakulima wanaweza
kuboresha ufanisi wa kazi zao kwa kupata maarifa ya kitaalamu yanayozingatia
tafiti na teknolojia za kisasa.
0 Comments