Na: Ayoub Mwigune
Polisi Wasaidizi wa Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA), limewahakikishia wanafunzi wanaotamani kujiunga
na Chuo hicho kuwa hali ya usalama ndani ya mazingira ya chuo ni shwari na kuwa
ulinzi umeimarishwa kwa kiwango cha hali ya juu ili kuhakikisha mazingira bora
ya kujifunzia na kuishi.
Akizungumza katika mahojiano maalum na SUA FM katika viwanja vya maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro, Msimamizi wa Polisi Wasaidizi SUA ambaye pia ni Msaidizi wa Kamishna wa Polisi (ACP), Simon Haule amesema askari wa SUA wamejidhatiti kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayekuja SUA anakuwa salama kwa wakati wote akiwa chuoni.
"Tunaendelea kuwajengea
uwezo askari wetu kupitia mafunzo na miongozo ya kiusalama, lengo letu ni
kuhakikisha kila mwanafunzi anasoma na kuishi katika mazingira ya amani bila
hofu yoyote kwani ulinzi hapa SUA si suala la bahati nasibu, ni wajibu wetu wa
kila siku," amesema ACP Haule.
Kwa upande wake, Mrakibu wa Polisi Msaidizi (SP) Nicholaus Mwamtobe ambaye ni Msaidizi wa Mkuu wa Idara ya Usalama SUA, amesema kuwa Chuo kimewekeza vya kutosha katika mifumo ya kiusalama ikiwemo doria za mara kwa mara, matumizi ya CCTV pamoja na ushirikiano na vyombo vingine vya usalama.
"Tumeimarisha doria usiku
na mchana, ndani na nje ya Chuo, na tumewahimiza wanafunzi kuzingatia miongozo
ya kiusalama inayotolewa na uongozi, huu ni mpango shirikishi ambao
tunautekeleza kwa weledi mkubwa," amesema SP Mwamtobe.
0 Comments