Na: Ayoub Mwigune
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuwa kinara wa mageuzi katika
sekta ya kilimo nchini kwa kutambulisha teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki
(drones) kwa matumizi ya kilimo, hususan katika usambazaji wa viuatilifu na
mbolea mashambani.
Akizungumza katika maonesho
ya Nanenane Kanda ya Mashariki wakati wa mahojiano maalum na SUA Media, Afisa
Kilimo wa SUA, Bi. Fatuma Hassan amesema matumizi ya ndege nyuki ni miongoni
mwa mbinu za kisasa zenye uwezo wa kuongeza tija kwa wakulima kwa usahihi na
ndani ya muda mfupi.
Amesema
teknolojia hiyo ina uwezo wa kupulizia dawa au mbolea katika eneo kubwa bila
mkulima kuingia shambani, hivyo kumuepusha na madhara ya moja kwa moja
yatokanayo na kemikali.
Bi. Fatuma ameongeza kuwa SUA imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo ya mbinu bora za kilimo pamoja na matumizi ya teknolojia mbalimbali ambapo kwa sasa, Chuo hicho kimeanza rasmi kutoa mafunzo maalum ya matumizi ya ndege nyuki kwa vijana wanaosomea kozi za kilimo, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili wakulima katika jamii na Taifa kwa ujumla.
"Teknolojia hii
inalenga kuongeza ufanisi katika shughuli za kilimo kwa kupunguza muda wa kazi,
gharama na athari za kiafya kwa wakulima," amesema Bi. Fatuma.
Aidha, amesema matumizi
ya teknolojia hiyo yamesaidia kupunguza gharama na muda wa kazi mashambani,
kulinda mazingira, na kuimarisha afya ya wakulima kwa kuwaepusha na athari za
moja kwa moja za kemikali.
0 Comments