Na: Josepuhine Mallango
Wahitimu
wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamekuja na Mfumo wa Afya ya Mnyama
Digital ambao umeelezwa kuwa ni muhimu na rafiki kwa maendeleo ya mashamba ya
wafugaji katika kuongeza uzalishaji na kipato sambamba na kusaidia kupunguza
gharama za uzalishaji.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Afya ya Mnyama Digital, Julieth Tarimo,
wakati akizungumza na SUA Media katika Maonesho ya Nanenane, ambapo amesema ni
muhimu zaidi kutumia mfumo wa Afya ya Mnyama Digitali ambao ni teknolojia ya
kuweka tagi ya kidigitali ya sikio (smart ear tag sensor) kwa sababu ni huduma
inayomsaidia mkulima kupata taarifa za maendeleo na kufuatilia kwa ukaribu
mnyama wake anapopata changamoto inamsaidia kupata taarifa sahihi na za haraka
na na hivyo kujua maendeleo ya mnyama wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Afya ya Mnyama Digitali, Mabula Marko, amesema mfumo wa kidigitali mpaka sasa umeshahudumia zaidi ya ng’ombe 1000 katika mikoa ya Morogoro, Kagera na Shinyanga kwa kuweka tagi ya kidigitali, na kwamba mfumo huo umetengenezwa kwa mazingira ya kitanzania zaidi ambapo unaweza kutumika katika mazingira yote ya vijijini na mjini.
Pia,
ukiwa mbali na mifugo yako, unafunga tagi ya sikio na bado una uwezo wa
kufuatilia mifugo yako popote unapokuwa, tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa
lazima uwe karibu na eneo la mifugo.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa faida ambazo ziko kwenye mfumo wa Afya ya Mnyama Digitali ni pamoja na mfugaji kupata taarifa za madaktari waliosajiliwa na Baraza la Madaktari Tanzania, kupata madawa na kiwango kinachoruhusiwa kutumika katika mashamba ili kuongeza uzalishaji unaotokana na ufugaji.
Amesema
gharama za mfumo ni shilingi 50,000/= kwa ng’ombe mmoja kuwekewa tagi ya
kidigitali ya sikio, ambapo kutokana na mazingira ya wafugaji wa Kitanzania
wameweka mazingira ya kulipia kidogo kidogo mpaka mfugaji anamaliza na kubaki na
tagi hiyo moja kwa moja.
Amesema
endapo mnyama atakufa, tagi hiyo inaweza kuhamishiwa kwa mnyama mwingine, hivyo
amewataka wafugaji kufika kwa wingi katika banda lao la Afya ya Mnyama Digital
ili kupata elimu na huduma ya afya ya mnyama kwa njia ya kidigitali.



0 Comments