SUAMEDIA

Malisho bora yatajwa kuwa suluhisho la migogoro ya wakulima na wafugaji

 Na: Vumilia Kondo

Wataalamu wa mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameeleza kuwa kilimo cha malisho bora ya wanyama kinaweza kuwa suluhisho la kudumu la migogoro inayojitokeza mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji nchini.

Akizungumza katika maonesho ya kilimo ya Nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro, Ahmed Amasha ambaye ni Afisa mifugo kutoka SUA amesema kuwa kupitia teknolojia ya kuzalisha malisho ya kisasa kwenye maeneo madogo, wafugaji wanaweza kupunguza utegemezi wa kutangatanga kutafuta chakula cha mifugo.

Amasha  amesema banda la mafunzo ya mifugo kutoka SUA limeonesha aina tatu kuu za malisho ambayo yanaweza kuleta tija kwa wafugaji bila kuathiri shughuli za kilimo.

“Tunayo malisho ya jamii ya mikunde kama Alfa Alfa na Russian Confrey ambayo yana protini ya kutosha na huongeza virutubisho kwa mifugo. Pia tunayo majani tembo kama Local Napia na Giant Juncao ambayo hustahimili ukame na kutoa mazao ya kutosha,” amesema Amasha.

Aina nyingine ya malisho iliyotajwa ni nyasi za malisho kama Rhodes, Brachiaria, Cencrus ambazo zinaweza kulimwa, kukatwa na kuhifadhiwa kama lishe ya wanyama hasa wakati wa kiangazi.

Kwa mujibu wa Amasha, baadhi ya majani hayo kama Giant Juncao yana uwezo wa kutoa mavuno hadi tani 180 kwa mwaka kwenye hekta moja na yana protini ya hadi asilimia 18, hivyo kusaidia kukuza mifugo ya maziwa na nyama kwa haraka.

“Kwa kutumia malisho haya, mfugaji anaweza kulisha mifugo bila kutoka nje ya shamba lake. Hii inaondoa migogoro na wakulima kwa sababu hakuna kutangatanga. Pia, malisho haya yanaweza kulimwa kibiashara na kuuza kwa wafugaji wengine,” ameongeza.

Aidha, ametoa wito kwa wafugaji kuanza kuwekeza kwenye kilimo cha malisho badala ya kuongeza idadi ya mifugo pasipo kuwa na uhakika wa lishe.

“Tunahamasisha wafugaji kulima majani haya ili wawe na mifugo michache yenye tija kuliko kuwa na makundi makubwa yasiyo na faida,” amesema.

Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa la kuonesha teknolojia mbalimbali za kilimo na mifugo huku SUA ikijitokeza kuhamasisha matumizi ya mbinu za kisasa katika ufugaji na uzalishaji wa chakula cha mifugo.






Post a Comment

0 Comments