Na: Vumilia Kondo
Wataalamu wa mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameeleza kuwa teknolojia ya ufugaji wa samaki wa jinsia moja inaweza kuongeza uzalishaji na kipato kwa wafugaji kwa muda mfupi.
Akizungumza katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro, Afisa Mifugo kutoka SUA, Dickson Tryphone, amesema kuwa Chuo hicho kupitia Idara ya Mafunzo ya Mifugo na Viumbe Maji, kimeleta teknolojia ya uzalishaji wa sato na kambale kwa kutumia mbinu za kisayansi zenye lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa samaki.
“Tunazalisha sato wa jinsia moja kwa kutumia homoni za kiume ambazo huwasaidia vifaranga kubadilika kuwa wa kiume pekee. Samaki wa kiume hukua haraka, kuwa na miili mikubwa, na hufikia uzito wa soko ndani ya miezi mitano hadi sita,” amesema Tryphone.
Kwa upande wa kambale, Tryphone amesema kuwa wazazi huzalishwa kwa kuchomwa homoni maalum kwa ajili ya kuharakisha ukomavu wa mayai, kisha mbegu za kiume huondolewa na kuchanganywa na mayai hayo ili kupata vifaranga.
Vifaranga hao hulelewa kwenye nasari kwa kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kupelekwa kwenye mabwawa au kuuzwa kwa wafugaji.
Amesema homoni zinazotumika katika kuzalisha samaki wa jinsia moja hazina madhara kwa afya ya mlaji, na zimepitishwa na mamlaka za kitaalamu kama salama.
“Wafugaji wengi hujiuliza kama hizi homoni zina madhara kwa binadamu, tunapenda kuwahakikishia kuwa hazina athari yoyote kiafya, zinatumika tu kubadili tabia za ukuaji wa samaki wachanga,” ameeleza.
Teknolojia hiyo imeelezwa kuwa na faida kwa sababu samaki wa jinsia moja hulishwa kwa kiasi kidogo cha chakula lakini hupata uzito wa soko kwa haraka, jambo linalosaidia kuongeza kipato cha mfugaji ndani ya muda mfupi.
Tryphone amesema SUA inaendelea kutoa elimu kwa wafugaji na jamii kwa ujumla ili teknolojia hiyo iweze kuwafikia wengi na kusaidia kukuza uchumi kupitia sekta ya ufugaji wa viumbe maji.



0 Comments