Na:
Josephine Mallango
Imeelezwa
kuwa wakulima wengi wa nguruwe bado wanakabiliwa na changamoto ya kutokujua
matumizi sahihi ya mbegu bora ili kupata tija, hususan mnyama kuwa na uzito
unaotakiwa wakati wa kupelekwa sokoni.
Hayo yameelezwa na Afisa Mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Stephano Kileo, wakati akitoa elimu ya mafunzo kwa wakulima wanaofika katika banda la Idara ya Sayansi ya Wanyama, Ukuaji Viumbe Maji na Nyanda za Malisho katika maonesho ya Nane Nane yanayoendelea mjini Morogoro.
Amesema
wakulima wengi wanaofika katika banda hilo kwanza wanaonesha hawajui aina ipi
ya mbegu bora wanayohitaji kutumia ili kupata tija kubwa katika ufugaji wa
nguruwe, ambapo wamekuwa wakitoa elimu ya kuwa na banda bora la kufugia, mbegu
bora, chakula sahihi cha kulisha mnyama na usimamizi yakinifu kwa maana ya
gharama za uendeshaji.
Afisa kilimo huyo kutoka SUA amesema ukiwa na mbegu bora ya nguruwe kama ya SUA aina ya Matured Boar (dume) na Gilf (jike), unapata mnyama ambaye anaongezeka zaidi nyama na kwa miezi sita anakuwa na kilo 90, uzito ambao unawavutia wanunuzi na hivyo kupata soko kirahisi.
Kwa upande wa chakula amesema nguruwe ni mnyama wa tumbo moja anayelishwa chakula kama dagaa, mashudu, madini, pumba za mahindi kwa mchanganyiko maalum ili mnyama aweze kupata tija unapompeleka sokoni, na kwamba wakulima wengi hawajui chakula kipi sahihi watumie kulisha nguruwe, wengi wao wanalisha majani na mabaki ya chakula.
Kileo
ameongeza kuwa kwenye chakula wanashauri mkulima anapomlisha mnyama ahakikishe
kila siku mnyama anakuwa na uwezo wa kuongezeka nusu kilo ya nyama, na hilo
linatokana na usimamizi wa shamba pamoja na mbegu bora ya nguruwe anayotumia.
Afisa kilimo huyo kutoka SUA amesema kuwa wakulima wanaalikwa kufika katika mabanda ya SUA ili kujifunza ufugaji wa nguruwe kibiashara. Ameongeza kuwa, iwapo mkulima hatafuata ushauri wa wataalamu, anaweza kupata hasara shambani kwake kwa sababu atatumia gharama kubwa katika ulishaji, lakini mnyama wake hataongezeka vizuri, hivyo atakumbana na changamoto ya kupata soko.
0 Comments