SUAMEDIA

SUA yaendelea na udahili wa Shahada za Uzamili na Uzamivu

 Na: Vumilia Kondo

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinaendelea na  dirisha la udahili kwa wanafunzi wa ngazi ya Uzamili na Uzamivu tangu Juni 12, 2025,  ikiwa ni tofauti na utaratibu wa miaka ya nyuma ambapo udahili huo ulianza mapema mwezi Aprili.

Kwa mujibu wa Theresia Merdad Afisa udahili  kutoka SUA, amesema udahili huo utaendelea hadi tarehe 6 Oktoba, 2025 ambapo baada ya hapo Chuo kitaanza mchakato wa usajili kwa wanafunzi waliokubaliwa kujiunga na programu mbalimbali.

Theresia amewahimiza wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi  kuwasilisha maombi yao mapema ili kupata nafasi katika kozi wanazozitaka.

Mbali na elimu ya darasani, SUA inajivunia kuwa Chuo kinachojikita kwenye mafunzo kwa vitendo ambapo wanafunzi hushiriki moja kwa moja katika tafiti na kazi za kiutendaji kupitia mashamba, maabara na vituo vya mafunzo vilivyopo chuoni.

Kwa upande wa sifa za kujiunga, waombaji wa shahada ya Uzamili wanapaswa kuwa na vyeti vya kidato cha nne, sita na shahada ya kwanza, wakati waombaji wa Uzamivu wanatakiwa kuwa na shahada ya kwanza na ya Uzamili, pamoja na nyaraka zingine kama cheti cha kuzaliwa na bima ya afya huku akibainisha kuwa kwa waombaji wa ndani ya nchi, cheti cha NIDA ni hitaji muhimu.

Chuo pia kimetangaza kuwa ada kwa wanafunzi wake ni nafuu ukilinganisha na vyuo vingine, na kimeweka utaratibu wa mwanafunzi kulipa robo tatu ya ada ili kuruhusiwa kujiandikisha, huku kiasi kilichobaki kikilipwa kwa awamu katika kipindi cha mwaka.

Aidha waombaji wanaruhusiwa kuchagua hadi kozi tatu tofauti wakati wa kuomba, jambo linalowapa nafasi kubwa zaidi ya kupata nafasi chuoni.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni miongoni mwa vyuo vinavyotambulika kwa kutoa elimu ya vitendo na kuandaa wataalamu wanaojiajiri na kuajiri wengine.

 

Post a Comment

0 Comments