SUAMEDIA

Vuyisile Mini SUA: Kiwanda kinachozalisha samani imara na rafiki kwa mazingira

 Na: Farida Mkongwe

Wananchi wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kutumia bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda cha kutengeneza samani cha Vuyisile Mini Furniture Factory kilichopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Solomon Mahlangu, Mazimbu mkoani Morogoro; bidhaa ambazo zina ubora wa hali ya juu na hutengenezwa kwa kuzingatia misingi ya utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu.

Mhadhiri Msaidizi, Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Mazao ya Misitu kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii SUA, Mbonea Mweta amesema kiwanda hicho kimekuwa msaada mkubwa katika kutoa huduma bora za uchakataji wa mbao, kukaushia na kutengeneza samani za kisasa zinazodumu kwa muda mrefu.

Amesema wananchi wanaopata huduma katika kiwanda hicho hupata bidhaa ambazo hazina matatizo kama mbao kupinda, kupasuka, au kushambuliwa na wadudu, matatizo ambayo mara nyingi husababishwa na mbao ambazo hazijakaushwa vizuri au kuchakatwa kwa kiwango duni.

Miongoni mwa mambo yanayokifanya kiwanda hicho kujitofautisha na viwanda vingine ni ukubwa wake na kuwepo kwa mashine zaidi ya 60 zinazofanya kazi kuanzia kuchana magogo, kukausha mbao, kuranda, kugereza, kufanya umaliziaji wa samani (finishing) hadi kufikia samani kamili.

Mbonea amesema kiwanda kinapokea magogo kutoka katika misitu endelevu ikiwemo Msitu wa Mafunzo wa SUA uliopo Olmotonyi mkoani Arusha, ambapo mbao hukatwa kwa uangalifu na kuchakatwa kwa viwango sahihi vya kitaalamu.

“Mchakato wote wa uzalishaji unafanyika ndani ya kiwanda chetu ambacho kimegawanyika katika maeneo maalum kama vile sehemu ya kuhifadhia magogo, kuchakata mbao, na kufanya finishing ya bidhaa, mbali na kuwa kituo cha uzalishaji, kiwanda pia kinatumika kama sehemu ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa SUA, watafiti na wananchi wanaotembelea kwa lengo la kujifunza au kupata huduma,” amesema Mbonea.

Kiwanda hiki kilianzishwa kwa heshima ya Vuyisile Mini, mwanaharakati wa Afrika Kusini aliyeongoza harakati za vyama vya wafanyakazi na aliyewahi kuishi katika maeneo ya Kampasi ya Solomon Mahlangu lakini kwa sasa, kiwanda hicho kipo chini ya SUA na kimekuwa kitovu cha ubunifu, ujuzi na uzalishaji bora katika sekta ya uchakataji wa mbao nchini.





Post a Comment

0 Comments