Na: Farida Mkongwe
Katika kukabiliana na changamoto sugu za magonjwa
yanayowaathiri wanyama na binadamu, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kupitia Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya kimeendelea kuibua
suluhisho bunifu kwa kutumia tafiti za kisayansi, utoaji wa huduma bora za
kiafya na ubunifu wa dawa asilia
Akizungumza katika banda la SUA kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mjini Morogoro, Prof. Claudius Luziga kutoka Idara ya Anatomia na Patholojia SUA amesema mwaka huu wamekuja na maonesho ya maeneo matatu makuu.
Moja kati ya maeneo hayo ni Hospitali ya Tiba ya Rufaa ya
Wanyama SUA, inayotoa huduma kwa wanyama wote wanaofugwa na wa porini ikiwa ni
pamoja na matibabu ya kisasa kama kutumia mashine za ultrasound, X-ray
na uchunguzi wa kina wa magonjwa ambayo hayawezi kutibiwa katika kliniki za
kawaida.
“Watu wengi wamekuwa wakituletea rufaa kutoka kliniki mbalimbali, kwa sababu sisi tuna vifaa na utaalamu wa hali ya juu,” amesema Prof. Luziga.
Eneo la pili ni mradi wa utafiti unaolenga magonjwa ambayo
hayapewi kipaumbele, hasa kifua kikuu cha wanyama (TB) na Brucellosis,
ambayo huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu ambapo mradi huo
unalenga kuondoa changamoto hizo kwa kushirikisha wataalamu wa afya kutoka
sekta mbalimbali.
“Katika maonesho hayo pia tunatoa elimu kuhusu changamoto ya vimelea sugu vya magonjwa vinavyoshindwa kutibika kwa dawa za kawaida ambapo SUA imejikita katika tafiti za kutumia miti tiba kutengeneza bidhaa kama sabuni, krimu na spray kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali ya ngozi kama fangasi, mapele, na majeraha ya moto”, amesema Prof. Luziga.






0 Comments