SUAMEDIA

Kilimo cha Malisho: Fursa ya ajira na uhakika wa chakula cha mifugo

 Na: Josephine Mallango 

Biashara ya kilimo cha malisho ni fursa nyingine inayotoa ajira kwa watu wasio wafugaji wala wakulima, sambamba na kuongeza upatikanaji wa malisho ya uhakika kutoka msimu mmoja kwenda mwingine.

Hayo yamesemwa na Daktari wa Mifugo Ahmed Amasha kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika viwanja vya maonesho Nanenane Kanda ya Mashariki katika banda la Idara ya Shamba kutoka Mazimbu wakati akizungumzia majani ya malisho yaliyopo katika banda hilo la SUA.

Amesema majani ambayo wameyaleta kwenye maonesho ni malisho ya ng'ombe ikiwemo majani ya Alfa Alfa, Bana Grass, Rashiani, Giant Juncao Grass, Local Napia, Congo Grass na majani makavu ambayo yanaweza kulimwa na mtu yeyote na mbegu zinapatikana, majani makavu yanaweza kuhifadhiwa kwa mwaka mzima na kutumika wakati wa kiangazi.

Ameongeza kuwa ufugaji wa ng'ombe unaongezeka kila kukicha na kwamba Serikali imekuwa ikitoa miongozo ya wafugaji kuwa na kundi la mifugo yenye tija ambapo sasa kupitia fursa hiyo watu wafike kwenye banda la SUA na kujifunza kilimo cha malisho ambayo ni rahisi ili waweze kulima na soko lake ni la uhakika kutokana na mahitaji ya wafugaji nchini.

Dkt. Amasha amesema wameshapata watu wanaotaka kuanzisha kilimo cha biashara ya malisho ikiwa ni pamoja na mdau kutoka Chalinze ambaye ana heka 200 na kwamba hata kwa mtu asiye na eneo kubwa anaweza kulima malisho kwa kutumia eneo dogo kwa kutumia majani jamii ya Alfa Alfa na Russian Comfrey ambayo yanatumika kama chakula cha kuongeza virutubisho katika ng'ombe, majani hayo yana kimo cha kufanana na matembele.

Amesema kuwa ulimaji wa malisho unaanzia kwa wafugaji wenyewe kulima na kuhifadhi malisho, pamoja na watu wengine kujihusisha na kilimo cha malisho kama biashara, unaweza kuwa njia mojawapo ya kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji na kwamba hatua hiyo itasaidia kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha mifugo kwa uhakika kutoka msimu mmoja hadi mwingine, hivyo kupunguza migogoro hiyo kwa kiasi kikubwa.




Post a Comment

0 Comments