SUAMEDIA

SUA yahimiza udahili wa mapema kwa programu mpya za ualimu wa amali

 Na: Hadija Zahoro

Wanafunzi, wazazi, walezi na wadau mbalimbali wa elimu wametakiwa kujitokeza mapema kufanya udahili, hasa katika programu mpya zilizoanzishwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kwa lengo la kukidhi mahitaji ya mtaala mpya wa elimu ya amali unaolenga kukuza ujuzi wa vitendo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari.

Akizungumza mubashara kupitia SUA FM katika banda la Udahili kwenye Maonesho ya Nanenane 2025, Afisa Udahili wa SUA, Grace Kihombo, amesema Serikali imeanzisha mtaala huo wa amali ili kuimarisha sekta ya elimu kupitia walimu waliobobea katika maeneo ya ufundishaji wa masomo ya vitendo.

Akieleza hatua ya SUA katika kuunga mkono juhudi hizo, Afisa Udahili huyo amesema Chuo hicho kimeanzisha programu mpya sita kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Amezitaja Programu hizo kuwa ni Shahada ya Ufundishaji wa Uzalishaji wa Mazao ya Kilimo (Bachelor of Crop Production with Education),  Shahada ya Ufundishaji wa Ushonaji na Mitindo ya Mavazi (Bachelor of Textiles and Clothing with Education na Shahada ya Ufundishaji wa Bustani na Mboga (Bachelor of Horticulture with Education).

Programu nyingine ni pamoja na Shahada ya Ufundishaji wa Lishe na Huduma ya Chakula (Bachelor of Nutrition and Catering with Education), Shahada ya Ufundishaji wa Ufugaji wa Viumbe wa Majini, (Bachelor of Aquaculture with Education) na Shahada ya Ufundishaji wa Uzalishaji wa Mifugo (Bachelor of Livestock Production with Education)

“Kozi hizi ni za muda wa miaka mitatu pekee na humwezesha mhitimu kupata ujuzi wa kitaaluma pamoja na sifa ya kuwa mwalimu wa elimu ya amali, hivyo ni fursa muhimu kwa vijana wenye nia ya kufundisha kwa vitendo,” amesema Grace.

Aidha, amewashauri wazazi, walezi na wanafunzi ambao hawajapata mwelekeo sahihi wa kozi wanazopaswa kuchagua kulingana na ufaulu wao kufika katika banda la udahili la SUA ili kupata ushauri wa kitaalamu.

Amesema taarifa zote kuhusu programu hizo zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya SUA ambayo ni www.sua.ac.tz, na udahili utafanyika kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, hivyo ni muhimu kwa waombaji kuhakikisha wanakamilisha hatua zote mapema na kwa usahihi.




Post a Comment

0 Comments