SUAMEDIA

SUA yawapokea Askari 11 waliohitimu mafunzo ya Ukaguzi wa Polisi Msaidizi

 Na: Hadija Zahoro

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimewapokea Askari 11 waliomaliza mafunzo ya kusomea cheo cha Mkaguzi wa Polisi Msaidizi (Assistant Inspector Course) yaliyolenga kuwaongezea utimamu, weledi na usasa katika masuala ya ulinzi na usalama wa raia katika maeneo yao ya kazi.

Mafunzo hayo yaliyoanza rasmi tarehe 23 Juni 2025 na kukamilika tarehe 15 Agosti 2025 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA) jijini Dar es Salaam, yalihusisha nyanja mbalimbali ikiwemo kudhibiti makosa ya jinai, masuala ya utawala, usimamizi wa majanga, haki za binadamu pamoja na mafunzo ya silaha.

Akizungumza na SUA Media mara baada ya hafla ya kuwapokea Askari hao, Kamishna Msaidizi wa Polisi na Msimamizi wa Polisi Wasaidizi wa SUA, ACP Saimon Haule, amesema Askari hao wamefaulu kwa kiwango cha juu jambo linalodhihirisha ubora wa utendaji wao wa kazi na litawasaidia zaidi katika usimamizi wa mali na ulinzi wa raia.

ACP Haule ameishukuru Menejimenti ya SUA ikiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa Askari wao, hususan katika kuwawezesha kupata mafunzo hayo.

“Ukiangalia rekodi kutoka mamlaka zote zinazotuma polisi wasaidizi kwenye vyuo vya Jeshi la Polisi Tanzania, SUA ndiyo inayoongoza kwa sababu menejimenti yake inatambua umuhimu wa mafunzo kama nguzo kuu ya rasilimali watu katika ulinzi,” ameongeza ACP Haule.

Kwa upande wao, Wakaguzi Wasaidizi akiwemo Inspekta Hamza Magolambo wa SUA Kampasi Kuu ya Edward Moringe, Inspekta Sabina Sumo na Inspekta Arold David Ngalya wa Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi, walmeishukuru Menejimenti ya Chuo na kuomba waendelee kupewa fursa za mafunzo.

Wamesema mafunzo hayo yamewaongezea nidhamu, weledi na uaminifu, huku wakiahidi kuyatumia kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa uadilifu na utaalamu.





Post a Comment

0 Comments