SUAMEDIA

SUA yaaga Baraza la 13, yakaribisha Baraza la 14 kwa Dira Mpya

 Na: Vumilia kondo

 Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanya mkutano maalum wa Baraza la Chuo kuaga rasmi Baraza la Chuo kwa Tathlitha ya 13 na kumaliza muda wa Mwenyekiti wake, Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman na  kukaribisha Baraza jipya la Chuo kwa Tathlitha ya 14.

Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chuo, wajumbe wa baraza, na wadau mbalimbali, ikiwa ni ishara ya mshikamano na mwendelezo wa maendeleo ya Chuo.

Akifungua hafla hiyo, Mkuu wa Chuo Mhe. Jaji Joseph Warioba   ametoa pongezi kwa Baraza la Chuo kwa Tathlitha ya 13 na hususan Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu Othmani Chande, kwa usimamizi bora katika kipindi cha miaka nane iliyopita.

Amebainisha kuwa SUA imepiga hatua kubwa , si tu katika mafunzo na utafiti, bali pia katika maboresho ya mazingira ya kujifunzia na kufanya kazi.

“Ingawa rasilimali zetu ni chache, tumepata matokeo makubwa kupitia usimamizi makini wa Baraza,” amesema,Jaji Warioba.

Aidha amesisitiza  kuwa elimu ndiyo chachu ya kuondoa umasikini na akahimiza mshikamano wa Baraza jipya na Menejimenti ya Chuo ili kuendeleza mafanikio.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti Mpya wa Barazala la Chuo kwa Tathlitha ya 14  Andrew Massawe , amempongeza Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Chande kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha SUA na kuahidi kuendeleza kazi nzuri iliyoachwa.

“Katika zama hizi za sayansi na teknolojia, tunahitaji ubunifu, mshikamano, na matumizi bora ya rasilimali ili kuhakikisha SUA inabaki kinara wa ubora kitaifa na kimataifa,” amesema.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibuda ametumia nafasi yake kumshukuru Mhe.Jaji Mkuu Mstaafu  Chande kwa uongozi wa mfano na kuwatambua wajumbe wote wa Baraza lililopita,  kwa msaada mkubwa katika masuala ya ushauri na uratibu na wizara husika.

Aidha, amesisitiza kuwa nguvu mpya kutoka Baraza jipya zinapaswa kuunganishwa na uzoefu wa wajumbe waliopo ili kuiwezesha SUA kusonga mbele.

Hafla hiyo imeacha alama ya mshikamano, heshima, na matumaini mapya kwa SUA kutokana na  ushirikiano wa viongozi, wajumbe wa baraza, na wadau, Chuo kimepanga kuendeleza nafasi yake kama kitovu cha elimu, utafiti, na ubunifu kwa maendeleo endelevu ya taifa.

 



Post a Comment

0 Comments