SUAMEDIA

Waziri Mkuu Majaliwa: Tunzeni kumbukumbu kwa maadili, uadilifu na usiri kwa usalama wa Taifa

Na: Mwandishi wetu

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watunza kumbukumbu nchini kuzingatia maadili ya kazi, kudumisha uadilifu na kulinda usiri wa taarifa, akisisitiza kuwa nyaraka ni nguzo muhimu kwa usalama wa Taifa na maendeleo ya nchi.

Akifungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema utunzaji bora wa kumbukumbu ni uti wa mgongo wa uwajibikaji, historia na utawala bora.

Amesisitiza kuwa TRAMPA ina jukumu kubwa la kuhakikisha nyaraka za Serikali na taasisi binafsi zinatunzwa kitaalamu, kwa usiri na usalama wa juu. Aidha, amezitaka taasisi za umma ambazo hazijaanza kutumia mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) kuanza mara moja, kwa kuwa Serikali imewekeza katika mifumo ya kidijitali ili kuongeza uwazi, kasi ya mawasiliano na kupunguza matumizi ya karatasi.

Waziri Mkuu pia ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kulipa madeni ya watumishi wa umma, ambapo hadi sasa shilingi bilioni 252.76 zimetolewa kwa watumishi 150,647, na shilingi bilioni 33.29 zimelipwa kwa wastaafu 10,022.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, amesema Serikali imetoa ajira mpya 965 kwa kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka mwaka 2024/2025, sambamba na kupandisha vyeo watumishi 1,237 na kuwabadilishia kada 59.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, amewapongeza wanachama wa TRAMPA kwa kulinda siri za ofisi kwa maslahi ya Taifa.

Amebainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inajenga jengo kubwa la kisasa la kuhifadhi kumbukumbu litakalozinduliwa hivi karibuni, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi ya kada hiyo katika majengo mapya ya Serikali.

Kwa upande wa washiriki, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeshiriki mkutano huo kwa kutuma jumla ya washiriki 13, mmoja kutoka Kampasi ya Mazimbu, mmoja kutoka Katavi na wengine 11 kutoka Kampasi Kuu ya Edward Moringe, Morogoro. Ushiriki huo umeonesha dhamira ya SUA kuunga mkono juhudi za kitaifa katika kusimamia na kuhifadhi kumbukumbu kwa weledi na kutumia teknolojia za kisasa.

Naye Mwenyekiti wa TRAMPA, Devota Mrope, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka.

Amesema Rais Samia amekuwa kiongozi wa mfano kwa kupigania maslahi ya watumishi wa umma, kutoa ajira nyingi na kushughulikia changamoto za kada hiyo.

Katika mkutano huo, wanachama wa TRAMPA walimkabidhi Rais gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya nchini.






Post a Comment

0 Comments