SUAMEDIA

SUA yawafundisha wanafunzi wa Mafiga kilimo kisichotumia udongo

 Na:Josephine Mallango.

Wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamebuni kilimo cha mjini cha mboga mboga cha mapambo kisichotumia udongo ambapo wanafunzi wa sekondari mkondo wa Amali kutoka Mafiga waliopo chini ya SUA wanashiriki katika kilimo hicho kuanzia mwanzo wa uzalishaji  mpaka kuvuna.

Kilimo hicho cha saladi ambacho wataalam wa SUA wamekilima kwenye chombo chenye muundo wa pambo ambalo wengi wamezoea kuyaona katika maua, kinatumia maji, makumbi na vifuu vya nazi ambavyo vimesangwa na kuwa unga ambao unga huo unaweza kutengeneza mwenyewe nyumbani au kununua madukani kwa kilo sh. 4000/= tu.

Akizungumza na SUA Media, Afisa Kilimo Mwandamizi kutoka SUA, Godwin Rwezaula, amesema wamekuwa wakiwafundisha wanafunzi wa sekondari Mafiga mkondo wa Amali mbinu shirikishi za kilimo cha mboga mboga mjini cha aina tofauti ikiwemo kilimo hicho kisichotumia udongo kutokana na mazingira ukizingatia wanafunzi hao wanatoka mjini.

Ameongeza kuwa kilimo hicho kinafanywa hata sehemu isiyo na udongo kabisa kwenye nyumba za kisasa za sasa zenye sakavu au vigae kwa kuwa hazichafui mazingira, ni kilimo rafiki na safi ambacho pia kinatumia muda mfupi kuanzia siku 21 mpaka 30 unakuwa umevuna saladi yako, kinaokoa muda wa kupatikana kwa mboga za majani nyumbani pia kinasadia kupunguza utapiamlo ambao unazikabili jamii nyingi.

Amesema lengo la kuanza na wanafunzi hao wa mkondo wa Amali kutoka Mafiga kuanzia hatua za awali za uzalishaji kwa vitendo inamjengea mwanafunzi tabia ya kuanza kuzalisha toka mdogo ili kumuwezesha kujitegemea na kuja kuwa mzalishaji mkubwa na kujiari mwenyewe badala ya kusubiri ajira, na kwamba kwa kipindi ambacho anasoma inampa hamasa ya kupata pesa ndogo ndogo za kujikimu.

Wanafunzi wa kidato cha pili 54 kutoka shule ya sekondari Mafiga wamekuwa wakijifunza kwa vitendo mbinu shirikishi za kilimo kutoka SUA  ambapo Rwezaula amesema kilimo hicho kinaweza kulimwa na mtu yeyote na kwamba wanashauri kabla ya kulima, kupata ushauri wa kitaalamu na ujuzi ambao ni mwepesi ili kupata tija wakati wa mavuno badala ya kulima kwa mazoea.






Post a Comment

0 Comments