Na:
Vumilia Kondo
Katika juhudi za kuhakikisha elimu ya utalii haiishii darasani, Idara
ya Utalii na Mapumziko huishi ya Chuo
Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) imeendelea kuandaa makambi ya mafunzo (camping)
kwa wanafunzi wake kama sehemu muhimu ya mafunzo ya vitendo.
Simmy Thadeo, Mkufunzi katika idara hiyo amesema camping ni zaidi ya
safari ya kawaida , ni jukwaa la kujifunza, kujitambua, na kujiandaa kitaaluma
katika mazingira halisi ya kazi.
“Camping ni sehemu ya mtaala wetu wa mafunzo, tunawapeleka wanafunzi
porini au kwenye maeneo ya vivutio vya utalii ili wajifunze kwa vitendo kila kitu
walichofundishwa darasani kuanzia upangaji wa safari, huduma kwa wageni, hadi
masuala ya mazingira na usalama,” anasema Thadeo.
Makambi hayo huandaliwa kwa muktadha wa mafunzo ya fani mbalimbali
ndani ya utalii, ambapo wanafunzi hupangwa katika timu na kupewa majukumu kama
walivyo wahudumu au waongoza watalii kwenye maeneo ya hifadhi au vivutio vya
asili.
“Kama hutaweza kupanga ratiba ya wageni, kupokea mgeni, au kujua namna
ya kuwahudumia vizuri , hujawa mtaalamu wa utalii, Camping inajenga stadi hizi
moja kwa moja,” amesisitiza.
Mbali na stadi za kitaaluma, wanafunzi hujifunza uongozi, kazi kwa
pamoja, na kutumia rasilimali chache kwa ufanisi, hii huwasaidia kujiandaa
kukabiliana na changamoto katika mazingira halisi ya kazi.
“Wanafunzi huandaa ratiba, hupika, hulala kwenye mahema, na kushughulika
na mazingira halisi ya kazi, ni uzoefu ambao hubadilisha namna wanavyoelewa
taaluma yao,” amesema Thadeo.
Kwa sasa, Idara inaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya
utalii na mazingira, huku ikiandaa wanafunzi wanaoweza kushindana katika soko
la ajira kwa ujasiri na weledi.
“Tunawaandaa kuwa si tu waajiriwa bora, bali pia wabunifu na watoa
suluhisho katika sekta ya utalii na mapumziko,” ameeleza Thadeo.
0 Comments