SUAMEDIA

SUA yatoa teknolojia ya mfumo mpya wa utambuzi wa chanjo na usajili wa mifugo

 

Na: Josephine Mallango 

 Maabara inayotembea kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye maonesho ya Nanenane mwaka huu 2025, inatoa fursa kwa  wananchi watakaofika kwenye banda la SUA  kujionea mfumo mpya wa utambuzi wa chanjo na usajili wa mifugo uliotengenezwa na SUA kupitia Taasisi ya SACIDS ambao  unalenga kutoa taarifa kwa haraka na kutatua kwa wakati nchi nzima .

Mfumo huo kwa sasa umeanza kutumika kwa ng’ombe ambao huvalishwa kifaa maalum kwenye masikio, kinachosomwa kwa skana  baada ya kupatiwa chanjo, taarifa zao zote huingizwa pamoja kwenye mfumo wa kidijitali unaoruhusu kusomwa kwa urahisi.

Serikali tayari imefanya uwekezaji kwa kuwapatia maafisa mifugo nchini vishikwambi pamoja na usafiri ili waweze kufika katika maeneo yote ya wafugaji kwa ajili ya kukusanya data.


Akizungumza na SUA Media Mratibu wa Maabara hiyo
  Dkt. Edson Kinimi amesema  magonjwa ya mlipuko  yana tabia ya kusambaa kwa kasi na kwamba SUA waliliona hilo na kuja na dhana ya  maabara inayotembea ili ugonjwa unapotokea waweze kuubaini na kutoa majibu kwa haraka ili kudhibiti magonjwa yasiende maeneo mengi na kusababisha hasara kwa nchi.

Amesema pamoja na tafiti wanazoendelea nazo  Maabara hii tayari imeshazunguka nchi nzima kuratibu na kubaini magonjwa ya mlipuko na majanga na kwamba maabara hiyo inayotembea ina uwezo mkubwa wa kupita katika maeneo yoyote hata maeneo  korofi  katika kipindi cha mvua.



"Tofauti na maabara nyingine, maabara hii ina vifaa vya kisasa vya
  utambuzi wa magonjwa ambavyo vina uwezo wa kuchukua sampuli na kuzifanyia kazi katika maeneo husika huko huko, vifaa vinavyoweza kugundua ugonjwa wowote ambao haujawahi kujulikana , kufika kwenye maeneo ambayo maabara nyingine hazifiki ikiwemo  maeneo ya migondi  na mapango ", amesema Dkt. Kinimi.

Ameongeza kuwa magonjwa ambayo mpaka sasa yameshatambuliwa na maabara hiyo inayotembea ni pamoja na Mgumba mkoani Lindi, Marburg mkoani Kagera, homa ya nguruwe, sotoka ya mbuzi na kondoo (ugonjwa ambao dunia imeweka mkakati wa kuukomesha ifikapo mwaka 2030), homa ya Bonde la Ufa, Chikungunya na unyong’onyevu wa mifugo. Aidha, tafiti mbalimbali bado zinaendelea, ikiwemo ile ya kupe, kwa kukusanya sampuli kutoka maeneo tofauti nchini.


Akizungumzia miongoni mwa mafanikio, amesema kuwa Tanzania imepongezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuweza kudhibiti ugonjwa wa Marburg uliolipuka mwezi Machi mkoani Kagera, ugonjwa hatari ambao mtu akiupata anaweza kufariki.

Hadi sasa ugonjwa huo umedhibitiwa na umekoma nchini, huku juhudi zikiendelea kupanua ushirikiano hadi kwa nchi za Korea na China, sambamba na kushirikiana na Maabara ya Taifa pamoja na wadau wengine wa ndani.




Post a Comment

0 Comments