SUAMEDIA

Mhe. Pinda avutiwa na ubunifu wa SUA katika Maonesho ya Nanenane 2025

 

Na: Farida Mkongwe

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo  Pinda, ametembelea Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Julius Nyerere, Nanenane 2025, na kujionea shughuli mbalimbali za kielimu na kiteknolojia zinazolenga kuboresha maisha ya wakulima na kuinua sekta ya kilimo nchini.

Mhe. Pinda ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, pamoja na viongozi wengine wa Serikali na kupokelewa rasmi na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, ambaye alitoa maelezo ya kina kuhusu tafiti, teknolojia na huduma mbalimbali zinazotolewa na SUA.



Prof. Chibunda ameeleza kuwa katika viwanja hivyo kuna takribani 48 yenye teknolojia na elimu mbalimbali ambazo zinalenga kumsaidia mkulima wa kawaida kwa kumuwezesha kutumia maarifa ya kisasa kwenye kilimo, ufugaji, lishe na afya ya wanyama.

Miongoni mwa maeneo aliyotembelea Mhe. Pinda ni banda la malisho ya mifugo, ambapo amepata maelezo kuhusu shamba la mfano la malisho lililopo SUA, pia ametembelea maabara inayotembea, ambayo imekuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko nchini, kwa uwezo wake wa kuchukua, kuchakata na kutoa majibu ya sampuli papo kwa papo kwenye eneo husika.

Maeneo mengine ambayo Mhe. Pinda ametembelea  ni Idara ya Lishe, ambako alipata taarifa kuhusu hali ya utapiamlo nchini na juhudi za SUA katika kukabiliana na changamoto hiyo, Hospitali ya Taifa ya Wanyama, pamoja na Shule ya Elimu ya Mafunzo ya Amali, ambako alipata maelezo kutoka kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mafiga, wanaosoma mkondo wa Amali kuhusu matarajio yao baada ya kumaliza masomo yao.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu ameweka historia ya kuwa miongoni mwa wageni wa kudumu wanaotembelea Banda la SUA kila mwaka anaposhiriki Maonesho ya Nanenane katika Viwanja vya Kanda ya Mashariki.





Post a Comment

0 Comments