SUAMEDIA

SUA yatajwa kuwa hazina kuu ya Kilimo Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki 2025

Na:  Josephine Mallango 

Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki, Morogoro, yana bahati ya kuwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo muhimu nchini kilichosheheni maprofesa na wataalam wengine wa kutosha wa kilimo na kwamba kilichobaki ni kwa viongozi wa Kanda ya Mashariki kutoka mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro  kushirikiana na SUA ili kuongeza tija katika kilimo.


"Nimetembelea banda la SUA, nimekuta kuna watoto wa shule ndiyo wanalima mboga mboga, Nimejionea teknolojia za hali ya juu na wale watoto wamepata hamasa ya kuahidiwa na Mkoa kupewa motisha ya shilingi laki moja kila mmoja akilima bustani ya kisasa nyumbani, nimejionea teknolojia wanazotumia, zinaleta tija katika kilimo.”

“ Maonesho haya ya Morogoro yana bahati ya kuwa na SUA ndani ya maonesho, Chuo muhimu kwa maendeleo ya kilimo, shirikianeni ili teknolojia na ujuzi huo uwafikie wananchi wa vijijini wa Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, walime kilimo cha tija, ni kilimo chenye manufaa," amesema Mhe. Pinda.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, ambaye kwa sasa ni Mshauri wa Rais katika masuala ya kilimo, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere mjini Morogoro, Agosti 2, 2025.

Mhe. Pinda amesema viongozi hao wa mikoa minne kutoka Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro wasilale, waungane kutafuta suluhisho la kudumu ili kusonga mbele katika sekta ya kilimo, uvuvi, ufugaji na misitu, kutokana na kuwa sehemu kubwa ya wananchi wamejiajiri katika sekta hizo kwa zaidi ya asilimia 65 hadi 70.

Ameongeza kuwa sasa kilimo kinahitaji kutumia dhana za kisasa ambazo zitaendelea kuongeza tija, kufuatia matumizi ya mbolea na mbegu bora nakwamba matumizi ya dhana za kisasa yatasaidia zaidi kuongeza tija huku akikemea kilimo cha jembe la mkono, akisema siyo rafiki kwa mazingira yaliyopo kwani kinafanya kilimo kuonekana kuwa ni kazi ngumu.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu amewataka viongozi wa Kanda ya Mashariki kuangalia fursa zilizolala ili waweze kuziamsha kwa ajili ya maendeleo ya nchi, kutokana na kuwepo kwa mapori mengi yanayonawiri.

Amesema kama mapori hayo hayawezi kutumika kwa kilimo, basi yatumike kwa ajili ya hewa ukaa, aidha, amesisitiza kuwa Maonesho ya Nanenane yasiwe jambo la mazoea tu kwamba yakifika tarehe yanafanyika, bali yatumike kuleta mawazo mapya ya kuboresha na kushauri ambapo ametoa pendekezo kuwa kila mwaka kifanyike kikao cha maandalizi kabla ya maonesho ili kuangalia yaliyofanyika, na tathmini ifanyike kila baada ya miaka mitano.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima amesema Maonesho ya Kanda ya Mashariki ndiyo bora zaidi nchini, na kwamba wanatarajia mahudhurio ya watu kuwa makubwa zaidi ukilinganisha na mwaka jana, kutokana na maandalizi yaliyofanyika kwa ufanisi mkubwa.

Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza katika maonesho hayo kutakuwa na banda la Mkoa litakalotoa mafunzo ya kilimo, uvuvi na misitu, ambapo kutakuwa na wataalam wa kutosha.

Mhe. Malima amesema lengo la maonesho hayo ni kujenga ukaribu zaidi na kuvutia watu mbalimbali, hususan wananchi wa mikoa ya Kanda ya Mashariki na mikoa mingine, kuja kujifunza kwa tija ili kuondokana na ile sura kuwa kilimo ni jambo gumu.

Kaulimbiu ya mwaka huu katika Maonesho ya Nanenane ni: Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.




  

Post a Comment

0 Comments