Na: Josephine Mallango
Serikali
imeombwa kuanzisha kituo maalum cha bidhaa zinazotokana na kilimo cha ikolojia
ili kumuwezesha mkulima kupata soko la uhakika.
Hayo yamesemwa na wakulima kutoka maeneo mbalimbali walioko katika maonesho ya Nanenane ndani ya mabanda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), hususan katika banda la Kitovu cha Kilimo Ikolojia, ambapo wamesema wamekuwa wakitekeleza kilimo kinacholinda mazingira kwa kutumia njia za asili, ikiwemo matumizi ya mimea tiba kwa kutibu mimea mingine.
Mkulima Juma Koba kutoka
Mgambazi, kata ya Magandu, wilaya ya Morogoro amesema wakulima wa kilimo cha
ikolojia wanakabiliwa na changamoto ya bei sokoni, ambapo bidhaa zao huuzwa kwa
bei sawa na bidhaa za kilimo cha kawaida, licha ya kuwa kilimo cha ikolojia
kinachukua muda mwingi na huzalisha mazao machache.
Naye Daudi Tesha,
mkulima kutoka wilaya ya Mvomero, amesema changamoto nyingine ni kwa walaji
wanapofika sokoni, mara nyingi huangalia mazao kwa muonekano wa nje tu, na mara
nyingine hayawavutii kwa sababu ya rangi au ukubwa, hali inayowafanya kupuuza
bidhaa za kilimo cha ikolojia.
Kwa
upande wake, mkulima Linah Wilson kutoka Gairo amesema kuwa Serikali inapaswa
kuwaangalia kwa karibu zaidi wakulima wa kilimo cha ikolojia kwa sababu ni
wachache na wanalima kwa njia salama inayotunza mazingira.
Ameongeza
kuwa kuanzishwa kwa kituo maalum cha masoko kwa mazao ya kilimo cha ikolojia
kutawanufaisha wakulima kwa kupata soko la uhakika, bei nzuri, na kuongeza
hamasa kwa wengine kulima kwa kutumia mbinu zisizotegemea kemikali za
viwandani.
0 Comments