Na: Hadija Zahoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kupitia Idara ya Maendeleo na Masomo ya Mkakati, Kitivo cha
Sayansi za Kijamii na Binadamu, kipo katika hatua za awali za kuandaa kanzi
data ya kijiografia (Land Resources and Conflict Geodatabase) yenye lengo la
kuchambua kwa kina sababu za migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa
mazingira na jamii.
Akizungumza na SUA Media katika viwanja vya maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mkoani Morogoro, Dkt. Edwin Ngowi, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara hiyo, amesema kuwa kwa mara ya kwanza SUA inajenga mfumo wa kanzi data wa aina hiyo utakaowezesha kuelewa kwa nini migogoro ya wakulima na wafugaji hutokea, hususan kwa kutumia mbinu za kijiografia.
“Tunaanza na mikoa ambayo
ina historia ya migogoro ya mara kwa mara, kama Morogoro hasa Wilaya za Kilosa
na Mvomero na baadaye tutahamia katika maeneo mengine kama Kiteto na katika
Mkoa wa Tanga ambapo jamii ya wafugaji wameonekana kuingia huko,” amesema Dkt.
Ngowi.
Dkt. Ngowi amesema kanzi
data hiyo itasaidia Serikali, hasa kupitia wizara husika, kufanya tathmini ya
maeneo yenye migogoro, kuelewa sababu kuu, na hatimaye kuweka mikakati ya
kuzuia migogoro hiyo kwa kiwango cha kitaifa.
Ameeleza kuwa hali hii
inatokana na jamii ya wafugaji kuishi katika maeneo yenye ukanda wa chini
ambayo huwa ya ukame, hivyo hulazimika kupeleka mifugo yao katika maeneo ya
wakulima yenye malisho bora na maji ya kutosha.
Amesema iwapo mradi huo
utazaa matunda kama inavyotarajiwa, kuna uwezekano mkubwa wa kanzi data hiyo
kuunganishwa na mfumo wa Wizara ya Mifugo ili kusaidia katika kupanga sera na
hatua za kudumu za kuondoa changamoto hiyo.
0 Comments