Na: Siwema Malibiche
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeibuka kidedea kwa kuwa Mshindi wa Jumla na Mshindi wa Kwanza katika
kundi la Taasisi za Mafunzo na Utafiti katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya
Mashariki yaliyofanyika mkoani Morogoro, kutokana na mchango wake mkubwa katika
sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza mara baada ya kupokea ushindi huo, Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda, amewapongeza wafanyakazi wote wa SUA kwa juhudi zao, akisisitiza kuwa ushindi huo umetokana na mchango wa Chuo katika kutoa elimu kwa jamii kupitia tafiti, teknolojia mbalimbali, na wataalamu wake bobezi wanaoleta chachu ya maendeleo katika sekta ya kilimo nchini.
“Mbali na mashamba darasa tunayotoa katika
maonesho haya, SUA pia tuna ndege isiyo na rubani kwa ajili ya shughuli za
kilimo hasa kwenye umwagiliaji wa mbolea na dawa, pia tuna maabara inayotembea
ambayo imekuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto za magonjwa kwa mifugo,
wanyamapori na binadamu,” amesema Prof. Chibunda.
Aidha, Prof. Chibunda ametoa rai kwa jamii kuendelea kukitumia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ili kujifunza kupitia tafiti na ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kuwa na kilimo chenye tija na kilimo biashara kwa maslahi ya taifa.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) na Mtafiti
kutoka SUA, Dkt. Devotha Mosha, amefurahishwa na ushindi huo na kuishukuru
Menejimenti ya Chuo kwa kuwezesha ushiriki mzuri kwenye maonesho pamoja na
kusisitiza jamii kuendelea kukitumia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ili
kufanikisha maendeleo katika kilimo na maisha kwa ujumla.
0 Comments