Na: Hadija Zahoro
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu
Ndemanga, amepokingeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa mchango wake
mkubwa katika kusaidia wakulima na wafugaji nchini kupitia tafiti za kisayansi
zinazolenga uzalishaji wa malisho bora kwa mifugo.
Akizungumza na SUA Media wakati akitembelea banda la SUA katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, Mhe. Ndemanga amesema SUA imekuwa msaada mkubwa kwa jamii, hususan kwa wakulima na wafugaji wanaokumbwa na changamoto ya upatikanaji wa malisho, jambo linalochangia migogoro baina ya makundi hayo.
“Tukiwa
viongozi ambao pia ni wakulima na wafugaji, tunathamini sana mchango wa SUA, tumeshuhudia
namna SUA inavyotoa elimu ya vitendo kuhusu uzalishaji wa malisho bora na namna
ya kuyaendeleza, hii ni elimu muhimu sana kwa wafugaji wa sasa,” amesema Mhe.
Ndemanga.
Amebainisha kuwa matumizi ya mbegu bora za malisho zinazotokana na tafiti za SUA yanaweza kuwasaidia wafugaji kuachana na mfumo wa kuhamahama wakitafuta malisho, na badala yake kutumia maeneo madogo kuzalisha chakula cha kutosha kwa mifugo yao.
“Kwa mfano,
ekari moja ya ardhi inaweza kugawanywa katika sehemu nne, kila sehemu inatumika
kwa zamu kulishia mifugo, na baada ya matumizi, sehemu hiyo inamwagiliwa ili
irejee katika hali yake ya kawaida, hii husaidia kuhakikisha chakula cha mifugo
kinapatikana mwaka mzima,” amesema Mkuu wa Wilaya.
Kwa upande wake SUA, imeendelea kutumia
tafiti na utaalamu wake kutoa suluhisho la kisayansi kwa changamoto ya malisho
kwa mifugo, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kusaidia kuboresha maisha ya
wakulima na wafugaji nchini, na kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya
makundi hayo.
0 Comments