SUAMEDIA

SUA yajivunia uzalishaji wa bidhaa bora zinazokidhi vigezo vya soko la kibiashara

 Na: Siwema Malibiche

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Kaya na Mlaji iliyopo Ndaki ya Kilimo SUA, kimetengeneza bidhaa mbalimbali za kibunifu zinazokubalika katika soko la kibiashara.

Akizungumza wakati wa maonesho ya wakulima yanayoendelea katika Kanda ya Mashariki, mkoani Morogoro, Mkufunzi Msaidizi kutoka Idara hiyo Mwanaidi Ally amesema SUA, kupitia studio yake ya ushonaji wa nguo na bidhaa za ngozi, huzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyokidhi soko la kimataifa.

Pia, amesema kuwa wanafunzi wanaosoma shahada mbalimbali zinazotolewa katika idara hiyo hupata ujuzi wa ubunifu unaowawezesha kujiajiri mara baada ya kuhitimu masomo yao.

"Ulimwengu wa sasa mavazi yamekuwa ni jambo kubwa sana, tofauti na zamani ambapo fundi cherehani alionekana kama mtu wa chini, leo hii kupitia sanaa ya mavazi, watu wanapata kipato kinachowasaidia kukidhi mahitaji yao ya kila siku," amesema Bi. Mwanaidi.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinaendelea kuikaribisha jamii kutembelea mabanda yake katika maonesho ya wakulima ya Kanda ya Mashariki, yaliyoongozwa na kaulimbiu isemayo: "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 2025."




Post a Comment

0 Comments