Na: Josephine Mallango
Mkufunzi na Msimamizi wa Mafunzo
ya awali kwa panya kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Priscus
Mramba, amesema kuwa panya wanaoshindwa kufuzu mafunzo yao, ambayo huchukua
kati ya miezi 8 hadi 9, hubadilishiwa aina ya mafunzo, na endapo watashindwa
kabisa, huwekwa katika eneo maalum la panya wazee na wastaafu, ambako huishi
hadi kufa kwao.
Akizungumza na SUA Media katika mabanda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mkufunzi huyo amesema kuwa pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia panya hao ambao hutumika kugundua mabomu katika nchi mbalimbali kama Kambodia, Azerbaijan, Angola, Ethiopia na Msumbiji, hapa nchini panya hao hutumika kwenye viwanja vya ndege kugundua nyara za Serikali.
Amesema
wakati wa mafunzo, baadhi ya panya hukumbwa na changamoto kama kuugua, ambapo hupatiwa
matibabu, na kwa wale wanaoshindwa kabisa kufuzu huchukuliwa kwa utaratibu
maalum, huwekwa kwenye mapumziko, hupewa mafunzo mbadala, na hupimwa kwa
majaribio mbalimbali ili kubaini uwezo wao wa kutambua sampuli endapo
wameshindwa hatua zote, hupelekwa rasmi kwenye eneo la wastaafu.
Mramba ameongeza kuwa kabla ya panya kupelekwa kwenye eneo la wastaafu, hufundishwa programu nyingine kwa mfano, kama ameshindwa kufuzu kwenye programu ya mabomu, anaweza kuhamishiwa kwenye programu ya utambuzi wa kifua kikuu (TB) au katika kazi za uzalishaji.
Amesisitiza kuwa panya hao
hawawezi kurudishwa porini kwani tayari wameingia kwenye kumbukumbu za
kimataifa za wanyama waliopitia mafunzo rasmi, hivyo hutunzwa hadi kufa kwao.
Amesema
panya wanaotumiwa katika mafunzo ya kugundua mabomu na kifua kikuu ni aina ya panya buku, na kwamba Watanzania wamekuwa
wakipewa kipaumbele katika nchi zote ambazo panya hao wamepelekwa. Aidha,
baadhi ya Watanzania wamepata ajira katika nchi hizo pale zinapohitaji huduma
ya panya waliopitia mafunzo hayo.
0 Comments