SUAMEDIA

SUA yajipanga Nane Nane 2025: Elimu, Teknolojia mpya, Udahili wa papo kwa papo

 Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimejipanga kikamilifu kuhakikisha kinatoa huduma mbalimbali zenye lengo la kuinua maisha ya wakulima, wafugaji, wanafunzi na jamii kwa ujumla ikiwemo huduma ya udahili wa papo kwa papo kwa wanafunzi wapya wanaotaka kujiunga na Chuo hicho maarufu nchini.

Dkt. Devotha Mosha, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) na Mtafiti kutoka SUA amesema mwaka huu Chuo kimekuja na tafiti na teknolojia mpya zilizotokana na kazi za hivi karibuni za watafiti wake, teknolojia ambazo zinalenga kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji nchini.

“Moja ya tofauti kubwa mwaka huu ni ukarabati mkubwa uliofanywa kwenye jengo letu na maeneo ya nje ya banda, mbali na maboresho hayo ya kimazingira, SUA imeleta teknolojia mpya kutoka kwa watafiti wake, zikiwemo za uzalishaji bora wa mifugo, ufugaji wa samaki na ushauri wa kitaalamu kuhusu mabwawa ya kisasa,” amesema Dkt. Devotha.

Ameongeza kuwa banda la SUA litatumika pia kutoa huduma ya udahili wa moja kwa moja kwa wanafunzi wapya na kusema hii ni fursa kwa wazazi, walezi na wanafunzi kutembelea banda hilo na kupata msaada wa karibu kuhusu taratibu zote za kujiunga na Chuo.

“Hii ni wiki ya udahili chuoni SUA, hivyo tunawakaribishaa wanafunzi wote wenye nia ya kujiunga nasi kufika kwenye banda letu ili kusaidiwa moja kwa moja,” ameongeza Dkt. Devotha.



Maonesho haya ya Nane Nane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere  Kanda ya Mashariki yatafunguliwa rasmi Agosti 2, 2025 na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda ambaye pia atapata nafasi ya kulitembelea banda la SUA kabla ya ufunguzi huo.



Post a Comment

0 Comments