SUAMEDIA

Kitovu cha Kilimo Ikolojia SUA chawajengea wakulima uwezo wa kulima bila kemikali

 

Na: Hadija Zahoro

Kitovu cha Kilimo Ikolojia kimeendelea kuwa kiunganishi muhimu kwa wadau mbalimbali wa kilimo hicho nchini, wakiwemo Mashirika, Serikali pamoja na watu binafsi ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwafundisha wakulima mbinu za kilimo ikolojia kwa lengo la kulinda afya za wazalishaji, watumiaji pamoja na mazingira.

Akizungumza na SUA Media katika banda la Kitovu cha Ikolojia SUA kwenye Maonesho ya 32 ya Nanenane 2025, Mtafiti Msaidizi kutoka Kitovu hicho kilichopo Idara ya Ugani na Maendeleo ya Jamii, Doris Shayo, amesema wakulima walioshiriki katika maonesho ya mwaka huu ni wale waliotolewa na wadau wa kilimo ikolojia ambao hufanya kazi moja kwa moja na wakulima hivyo imekuwa rahisi kwao kuzungumza lugha moja na kufundishana kwa ufanisi.

Mtafiti huyo amesema badala ya watafiti peke yao kuwaeleza wakulima kuhusu faida za kilimo ikolojia, wanawahimiza wakulima kutembelea banda la Kilimo Ikolojia ili kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wenzao wanaotekeleza mbinu hizo kwa vitendo katika maeneo yao na kwa lugha wanayoielewa.

Aidha, amesema kuwa ili kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na kilimo ikolojia, Kitovu cha Kilimo Ikolojia kwa sasa kinafanya kazi na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (Sustainable Agriculture in Tanzania SAT) ambalo hununua mazao hayo moja kwa moja kutoka kwa wakulima na kuyauza kwa bei nzuri ndani na nje ya nchi.

“Kwa sasa tunafanya kazi na SAT (Sustainable Agriculture in Tanzania) ambao wamechukua hatua ya kwenda kwa wakulima na kununua mazao moja kwa moja kutoka kwao, lakini pia wameweza kutengeneza vikundi vya wakulima ambavyo vina sauti moja ya kuuza kwa bei nzuri zaidi,” amesema Doris.

Kwa upande wake, Juma Koba, mkulima mdogo kutoka Kikundi cha Faraja Mgambazi kilichopo SUA mkoani Morogoro, amesema kilimo ikolojia ni rafiki kwa mazingira kwani hakitumii kemikali yoyote katika uzalishaji wake, bali hutegemea mboji na samadi zinazotokana na mabaki ya mimea.

Ameongeza kuwa wakulima wa kilimo ikolojia hutumia mimea dawa kama mipapai na pilipili kichaa, ambapo hupondwa, kuchanganywa na maji na kisha kupulizwa kwenye mimea ili kusaidia kuzuia wadudu na magonjwa, na hivyo kutoa mazao bora na salama kwa matumizi ya binadamu.





Post a Comment

0 Comments