Na: Josephine
Mallango
Imeelezwa kuwa
panya wa mashambani wanaoharibu nafaka wana uwezo mkubwa wa kuzaliana kwa
pamoja hadi kufikia watoto 18 kwa wakati mmoja, hali inayopelekea kuzuka kwa
milipuko mikubwa ya panya mashambani na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao.
Akizungumza na SUA Media katika maonesho ya Nane Nane yanayoendelea, Khalid Kibwana, Msaidizi wa Ofisi kutoka banda la Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu SUA, amesema taasisi hiyo inajihusisha na utafiti na udhibiti wa aina mbalimbali za panya, wakiwemo wale wa mashambani na wale wa ndani.
Ameeleza kuwa panya wa mashambani, akiwemo aina ya kindi, wanaweza kufanya uharibifu mkubwa kwa
mazao yakiwa shambani, hususani mahindi yanapokuwa katika hatua ya kukomaa, kutokana
na uwezo wao mkubwa wa kuzaliana, wanapaswa kudhibitiwa mapema kabla ya
kusababisha hasara kubwa kwa wakulima.
Kuhusu panya wa ndani, Kibwana amesema wamekuwa wakiharibu bidhaa za thamani kama fedha, nyaraka muhimu, pamoja na miundombinu ya umeme katika nyumba.
Aidha, ameeleza kuwa si panya wote ni waharibifu,
kwani kuna panya weupe wanaotumika katika tafiti mbalimbali vyuoni na hata
kwenye shule za sekondari kwa majaribio ya wanafunzi wanaosomea sayansi.
Panya hao wamekuwa
na faida kwa jamii ikiwemo kuchangia pato la taifa kupitia fedha za kigeni
kutoka kwa wanafunzi wa kimataifa, kutoa ajira kwa wahudumu wa panya, na kwa
jamii nyingine hutumika kama kitoweo kwa binadamu na chakula kwa wanyama.
Akizungumzia viumbe waharibifu wengine, Kibwana amesema fuko ni mharibifu mkubwa wa mazao ya mizizi kama viazi, mihogo, migomba na miti, huku ndege aina ya bundi akitajwa kuwa ni miongoni mwa njia asilia za udhibiti wa panya mashambani.
Kibwana amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa
wakulima juu ya mbinu mbalimbali za kudhibiti panya na viumbe hai waharibifu
kwa kutumia mitego maalum, pamoja na njia za kuhifadhi mazao kwa usalama kama
kutumia mifuko ya kinga njaa na madumu maalum ili kuzuia hasara baada ya
mavuno.


.jpg)
.jpg)
0 Comments