SUAMEDIA

SUA yaanzisha App ya Mkulima ili kurahisha upatikanaji wa machapisho ya maarifa

 Na: Josephine Mallango 

Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo (SUA) imebuni App ya Mkulima ambayo inamsogezea mkulima huduma ya machapisho mbalimbali moja kwa moja kupitia simu ya mkononi, ikiwa ni jitihada za kuendelea kuboresha upatikanaji wa taarifa za uzalishaji bora na kuongeza mapato.

Akizungumza na SUA Media, Jabir Jabir, Mkutubi na Msimamizi wa Kitengo cha Rejea na Machapisho kwa Jamii kutoka SUA, amesema wameendelea kuboresha Mkulima Collection katika ghala la taarifa kwa ajili ya watumiaji wa kompyuta, na sasa wametengeneza app hiyo ili kuwasogezea taarifa zaidi wale wanaotumia simu.

Amesema app hiyo, ambayo tayari ipo katika Play Store, imerahisisha upatikanaji wa taarifa ambapo mtumiaji anaweza kuipakua, kuifungua, na kuona machapisho mbalimbali ya maarifa kwa urahisi kupitia simu ya mkononi.

Mkutubi huyo amewahimiza wananchi kujenga tabia ya kusoma na kupata maarifa mapya kwani Maktaba ni chombo kinachokua kila siku, na elimu inaendelea kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na teknolojia mpya zinazojitokeza.

Amesisitiza kuwa usomaji wa taarifa ni muhimu kwa sababu maarifa yanabadilika kwa kasi, hivyo kutumia taarifa zile zile za zamani kunaweza kusiwe na tija na kwamba kwa kutumia app hii, wakulima na wananchi wataweza kupata maarifa yanayokwenda na wakati na hivyo kuongeza uzalishaji na ufanisi.

Maktaba ya Taifa ya SUA inahudumia wanafunzi, watafiti, na jamii kwa ujumla, ambapo katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki huduma hutolewa kupitia Mkulima Collection, inayopatikana kwa njia ya machapisho ya nakala ngumu na pia kupitia tovuti ya SUA .

Post a Comment

0 Comments