SUAMEDIA

Mradi wa Interact Africa waimarisha ushirikiano wa kimataifa SUA

Na: Ayoub Mwigune 

Mradi wa Interact Africa unaoendeshwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu na utafiti kwa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wataalamu mbalimbali.


Hayo yameelezwa na Dkt. Jacqueline Makatiani, ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Moi na Mratibu wa Mradi wa Interact Africa, wakati akizungumza katika hafla ya kukutana na wadau wa mradi huo chuoni SUA.

Dkt. Makatiani amesema utekelezaji wa mradi huo unahusisha vyuo vikuu na taasisi mbalimbali barani Afrika na pia nje ya bara hilo, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika sekta za kilimo, afya na mazingira.

Amesema mradi huo umekuwa chachu ya kukuza ujuzi wa wataalamu kwa njia ya mafunzo ya vitendo, warsha na miradi shirikishi inayohusisha wanafunzi, wahadhiri na watafiti, “lengo letu ni kuhakikisha SUA inakuwa kiungo muhimu cha utafiti na uvumbuzi unaoweza kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi,” ameeleza.

Aidha, amefafanua kuwa Interact Africa inalenga kuimarisha mitandao ya kitaaluma kati ya SUA na vyuo vingine vinavyoshirikiana, hatua inayowezesha tafiti zenye matokeo chanya kwa maendeleo ya jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walionufaika kusomeshwa na mradi huo, akiwemo Hillen Lumbu pamoja na Joyce Nyambura waliowakilisha wenzao, wameushukuru mradi huo kwa kuwasaidia kielimu na kuwapa uzoefu wa kitaalamu ambao umeongeza ujuzi na kuandaa mazingira bora kwa mustakabali wao wa kitaaluma.

Kwa upande wake, Mgeni Rasmi Prof. Maulid Mwatawala, ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA Prof. Raphael Chibunda, amesema SUA imeboresha mitaala yake yote ili iwe ya msingi wa umahiri, ikijumuisha masomo kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ujumuishi, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia mpya, ikiwemo akili bandia (AI).







Post a Comment

0 Comments