Na: Farida Mkongwe
Magonjwa
yasiyoambukiza yanayotokana na lishe duni ni magonjwa ambayo hayasababishwi na
vimelea kama virusi au bakteria, bali husababishwa na mitindo ya maisha
isiyofaa.
Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Lishe na Sayansi ya Mlaji, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Hasna Bofu amesema kutofanya mazoezi ya mwili, ulaji usiozingatia lishe bora na matumizi ya vyakula vilivyosindikwa vimechangia kuongezeka kwa magonjwa haya katika jamii.
Kwa mujibu wa takwimu za
Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2024, takribani asilimia 70 ya vifo vyote
duniani vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la
damu, magonjwa ya moyo na saratani.
“Hapo awali magonjwa haya yalikuwa yakiathiri zaidi watu wazima, lakini kwa sasa yameanza kuonekana hata kwa vijana na watoto wadogo kutokana na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi na chumvi kupita kiasi”, amesema Mhadhiri huyo.
Ameongeza kuwa pamoja na
ulaji usiofaa, kutofanya mazoezi kunachangia sana kuongezeka kwa uzito na
hatimaye kusababisha magonjwa haya ambapo ili kujikinga, ni muhimu kufanya
mazoezi angalau kwa dakika 30 kila siku na kuhakikisha unazingatia ulaji wa
vyakula kutoka makundi yote sita ya lishe.
Amevitaja
vyakula hivyo kuwa ni pamoja na vyakula vyenye asili ya mizizi, mikunde,
mbogamboga, matunda, vyakula vya asili ya wanyama kama vile dagaa na mayai,
pamoja na mafuta yenye asili bora.
0 Comments