Na: Josephine Mallango
Wahitimu
wa Shahada ya Familia na Afya ya Mlaji pamoja na Shahada ya Maendeleo ya Jamii
kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamesherehekea kwa shangwe
kumaliza mitihani yao ya mwisho, wakifurahia mafanikio yao kwa burudani
mbalimbali chuoni hapo huku wakitoa shukrani kwa walimu waliowaongoza katika
safari yao ya kitaaluma.
Wakizungumza baada ya kumaliza mitihani yao, baadhi ya wahitimu wameeleza namna wanavyojipanga kujiajiri wakisubiri Maafali yanayotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Irene Paul
Emanuel,
mhitimu wa Shahada ya Familia na Afya ya Mlaji, amesema amejiandaa kuingia moja
kwa moja kwenye ujasiriamali kwa kutumia kipaji chake cha upambaji (makeup).
"Siwezi
kurudi nyumbani nikae, nataka nikifika nyumbani nanunua vifaa vya makeup na kuanza kazi, walimu wetu
wametufundisha kuwa wabunifu na kujitegemea, nitajitangaza kupitia mitandao ya
kijamii na kuwafuata wateja wangu kokote walipo kwa sababu nimefundishwa
kitaalamu, nitatoa huduma ya kiwango cha juu tofauti na watu wanaopaka makeup kwa mazoea. Najua nitafanikiwa
kabla ya maafali,” amesema Irene.
Kwa upande mwingine, Happiness Shababi Sillo, ambaye pia ni mhitimu wa Shahada ya Familia na Afya ya Mlaji, amesema ujuzi alioupata chuoni umemfungulia milango mingi ya kujiajiri.
"Nimejifunza
kushona viatu, mabegi, nguo za aina mbalimbali, pamoja na kutengeneza mapambo
ya ndani ya nyumba, shule na kwenye shughuli za chakula (catering), nina uwezo
wa kutengeneza mapambo ya kipekee na kupanga mazingira ya kuvutia, huu ujuzi
unaweza kunifanya niajiriwe au nijiajiri mwenyewe," amesema kwa matumaini
makubwa.
0 Comments