Na: Farida Mkongwe
Wananchi kutoka mikoa ya Tanga,
Pwani, Dar es Salaam na Morogoro wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki
Maonesho ya Kilima, Ufugaji na Uvuvi
(Nane Nane) Kanda ya Mashariki, yatakayofanyika katika Viwanja vya
Mwalimu Julius Nyerere, mjini Morogoro kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, amesema miongoni mwa vivutio vikubwa vya mwaka huu ni kuanzishwa kwa Jukwaa la Business & Education, litakalotoa mafunzo bure kwa wananchi kupitia mada mbalimbali zinazohusu kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Mwaka huu tumeongeza msukumo
katika elimu kwa vitendo. kupitia jukwaa hili, wananchi wataweza kujifunza kila
siku kutoka kwa wataalamu waliobobea kutoka taasisi za Serikali na sekta
binafsi,” amesema Mhe. Malima.
Kwa mujibu wa ratiba ya kamati
ya maandalizi ya maonesho hayo ufunguzi rasmi utafanyika tarehe 2 Agosti 2025
na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu mstaafu Mhe, Mizengo Pinda.
Mhe. Malima amesema licha ya
changamoto zilizojitokeza katika miaka iliyopita, ikiwemo upungufu wa maji,
mwaka huu hali ni tofauti, “tumechimba kisima kwa kushirikiana na Wizara ya
Maji, tumehakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika,” amesema Malima.
Halmashauri zote kutoka mikoa
ya Kanda ya Mashariki zinatarajiwa kushiriki katika maonesho hayo, pamoja na
taasisi za utafiti, vyuo , mashirika ya maendeleo na wadau mbalimbali wa sekta
ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na
wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali watashiriki kuonesha bidhaa
na huduma zao.
Maonesho hayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kutoa
elimu, kuhamasisha matumizi ya teknolojia, kubadilishana maarifa na kuonesha
mafanikio katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
0 Comments