Na: Josephine Mallango
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khalid Masoud Wazir, amesema kuwa fursa zinazopatikana katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ni muhimu sana na zinapaswa kutangazwa zaidi, kwani zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
Amesema hayo wakati wa majumuisho ya ziada ya siku chuoni SUA, ambapo ametembelea baadhi ya vitengo muhimu vya Chuo hicho vikiwemo Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Uchumi wa Buluu, Kitengo cha Mifugo, Kitengo cha Bustani, Jengo Mtambuka la Mafunzo la Dkt. Samia, Kitengo cha Teknolojia ya Kufundishia, SUGECO, pamoja na Kituo Atamizi cha Vijana.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema
SUA ina majibu ya mikakati ya
utekelezaji wa Serikali zote mbili kwa kuwa inawaongezea wataalam ujuzi na
kutoa ajira kwa vijana za kujiajiri wenyewe kutokana na mitaala yao na
ufundishaji uliojaa vitendo unaosababisha vijana wanaoamaliza kuwa na uwezo wa kujiajiri.
“Hiki Chuo namna nilivyofika na nilivyotembea imenipa mtazamo tofauti na awali ni Chuo kikubwa mno na kina majibu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali hasa kule Zanzibar kuna suala la uchumi wa bluu umefanyika uwekezaji mkubwa na umekamilika ila imebaki suala la ujuzi bado tuna wataalam wachache lakini kwa namna nilivyoona hapa SUA ufugaji wa samaki , kilimo ikiwemo cha matikiti maji na mboga mboga, haya mambo yazidishiwe kutangazwa ili yafike kila mahala yataendelea kusaidia utatuzi wa uchumi wa nchi ”, amesema Mhe. Wazir.
Kutokana na umuhimu wa elimu ya vitendo kwa maendeleo ya
uchumi wa buluu na sekta ya kilimo, Naibu Katibu Mkuu huyo ameuomba uongozi wa
SUA kuanzisha kampasi ya SUA Zanzibar
ili kusaidia vijana wengi zaidi kupata ujuzi unaohitajika kwa wakati huu.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA, Prof. Raphael Chibunda, alisema kuwa kwa sasa SUA ina ushirikiano wa karibu na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), na kwamba idadi ya wanafunzi kutoka Zanzibar wanaojiunga na SUA inaongezeka mwaka hadi mwaka.
Prof. Cibunda amesema SUA kinaendelea
kuwa Chuo cha mafunzo kwa vitendo na wahitimu
kutoka SUA wana uwezo wa kujiajiri wenyewe ama kuajiriwa na kuweza kuingia katika
ushindani wa soko la ajira popote
kutokana na wanavyoandaliwa chuoni hapo .
0 Comments