Na: Farida Mkongwe
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetangaza rasmi mitaala mipya sita
inayolenga kuwaandaa walimu wa kufundisha masomo ya amali katika shule za
msingi na sekondari, kufuatia mabadiliko makubwa ya sera ya elimu na mitaala
nchini.
![]() |
Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) |
Akizungumza
na waandishi wa habari Julai 22, 2025 chuoni hapo, Makamu Mkuu wa SUA, Prof.
Raphael Chibunda, ameeleza kuwa mitaala hiyo mipya imeundwa kwa weledi mkubwa
ili kuhakikisha Taifa linapata walimu stadi watakaoendana na mabadiliko ya
mfumo wa elimu unaolenga kutoa maarifa na ujuzi kwa vitendo.
“Leo tumewaita mahususi kuwaeleza
watanzania kuhusu kuanzishwa kwa mitaala mipya sita inayojibu mahitaji ya
mabadiliko ya elimu nchini, hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha tunaandaa
walimu mahiri wa kufundisha masomo ya amali kwenye shule zetu,” amesema Prof. Chibunda.
Prof. Chibunda amesema mitaala hiyo mipya imeshaidhinishwa
na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kwamba SUA inakuwa Chuo cha kwanza
kutekeleza maagizo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuandaa mitaala na kufundisha walimu wa masomo ya amali baada ya kubainika kwa changamoto kubwa ya
uhaba wa walimu wenye sifa na ujuzi wa kufundisha masomo hayo.
Ameitaja
mitaala hiyo kuwa
ni Shahada ya Ufundishaji wa Uzalishaji
wa Mazao ya Kilimo (Bachelor of
Crop Production with Education), Shahada ya Ufundishaji wa Ushonaji na Mitindo
ya Mavazi (Bachelor of Textiles
and Clothing with Education na Shahada
ya Ufundishaji wa Bustani na Mboga (Bachelor of Horticulture with Education).
Mitaala mingine ni
pamoja na Shahada ya Ufundishaji wa Lishe na Huduma ya
Chakula (Bachelor of Nutrition
and Catering with Education), Shahada
ya Ufundishaji wa Ufugaji wa Viumbe wa Majini, (Bachelor of Aquaculture with Education) na Shahada ya Ufundishaji wa Uzalishaji wa
Mifugo (Bachelor of Livestock
Production with Education)
Kwa
upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa
kitaalamu, Prof. Maulidi Mwatawala amesema kuzinduliwa kwa programu mpya za Shahada
zinazochanganya ualimu na stadi za amali ni hatua kubwa ya kimkakati itakayokuza
na kuchochea ajira na ujasiriamali nchini.
![]() |
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalamu, Prof. Maulidi Mwatawala akizungumza katika mkutano huo |
“…..mitaala
yetu kama tulivyosema sehemu kubwa ni mafunzo kwa vitendo wanajifunza ualimu
lakini anajifunza kwa vitendo zile stadi zenyewe za kilimo kwa hiyo ukiacha
kuajiriwa hata yeye mwenyewe ana uwezo wa kujiajiri kwa sababu atakuwa na stadi
za kutosha ambazo anaweza kutumia kuanzisha miradi mbalimbali iwe ya kilimo iwe
ya mifugo….”, amesema Prof. Mwatawala
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Masomo ya Shahada za Awali kutoka
SUA Dkt. Hamis Juma Tindwa,
amewahimiza waombaji wa nafasi za masomo
kuwasilisha maombi yao kwa njia rahisi na ya kidijitali kupitia tovuti rasmi ya
Chuo hich0 ambayo ni www.sua.ac.tz,
ambapo watakutana na maelekezo ya namna ya kuomba huku akiwataka wasisite
kuwasiliana na Chuo kwa msaada, akisisitiza kuwa SUA iko tayari kuwaongoza
kufanikisha ndoto zao za kitaaluma.
![]() |
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Masomo ya Shahada za Awali kutoka SUA Dkt. Hamis Juma Tindwa akifafanua kuhusu Mitaala mipya |
0 Comments