Na:
Hadija Zahoro
Kuelekea muhula mpya wa masomo
2025/2026, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Idara ya
Maikrobaolojia, Parasitolojia na Bioteknolojia kimewataka waombaji wa kozi ya
Shahada ya Sayansi ya Bioteknolojia na Sayansi za Maabara (BLS) kuhakikisha
wanakamilisha mchakato wa maombi mapema, kutokana na ongezeko kubwa la
wanafunzi wanaotaka kujiunga na programu hiyo.
Akizungumza mubashara kupitia kipindi
maalum cha udahili kwa wanafunzi kinachorushwa na SUA FM,
Mkuu wa Idara hiyo, Dkt. Augustino Alfred Chengula amesema kuwa kozi hiyo
hutolewa SUA pekee nchini na ina nafasi kubwa ya kumuwezesha mhitimu kujiajiri au
kuajiriwa.
Dkt. Chengula amesema Chuo kina uwezo
wa kudahili takribani wanafunzi 100 wa moja kwa moja kutoka ngazi ya kidato cha
sita na wanafunzi 40 kutoka ngazi ya stashahada, lakini kutokana na ongezeko la
waombaji na mahitaji ya kitaaluma, SUA imekuwa ikiongeza udahili hadi kufikia
wanafunzi 200 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa kozi ya Sayansi ya Bioteknolojia na
Sayansi za Maabara inajikita katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye
viumbe hai, hasa vimelea, kwa lengo la kuboresha maisha ya kila siku ya
binadamu na wanyama.
Aidha, wahitimu wa programu hii
huandaliwa kitaaluma na kwa vitendo kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya
maabara, zikiwemo hospitali, kliniki za wanyama, taasisi za utafiti, na pia
kujiajiri kwa kufungua maabara binafsi.
‘‘Tunatoa elimu ambayo imejikita zaidi
kumuwezesha mhitimu aweze kufanya kazi kwa vitendo pale anapomaliza ndiyo maana
tunasema kwamba si lazima aende VETA kwani ujuzi anaopata hapa unajitosheleza
kabisa kumuwezesha kwenda kufanya kazi moja kwa moja bila kupata changamoto
yoyote’’ amesema Dkt. Chengula.
Programu ya Shahada ya Sayansi ya
Bioteknolojia na Sayansi za Maabara (BLS) ilianza kutolewa rasmi SUA mwaka 2004, ikichukua muda wa miaka mitatu hadi kuhitimu ambapo tangu
kuanzishwa kwake, imekuwa kivutio kwa waombaji wengi nchini kutokana na umahiri
wa wahitimu wake ambao wameendelea kufanya vizuri katika sekta mbalimbali.
0 Comments