SUAMEDIA

SUA yaendelea kutekeleza mradi wa HEET kwa kasi, weledi na ubora

 Na: Siwema Malibiche

Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ikiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, imetembelea na kukagua mwenendo wa utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ambao unaendelea vizuri kuelekea kukamilika kwake.

 Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda (kulia) akipewa maelezo ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa HEET (Picha zote na Ayoub Mwigune)

Akizungumza na SUA Media Julai 22, 2025 wakati wa ziara hiyo katika Kampasi za Solomon Mahlangu na Edward Moringe mkoani Morogoro, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Utawala na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa, amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya kazi inayofanyika na amesisitiza kuwa wakandarasi wanapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji huku wakizingatia weledi na viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Prof. Muhairwa amebainisha kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia kati ya asilimia 20 hadi 40, na kuongeza kuwa moja ya faida kuu zinazotarajiwa kutokana na mradi huo ni kuongezeka kwa miundombinu ya kisasa kama vile madarasa ambayo yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

 Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphaeli Chibunda (kulia) akiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Utawala na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa (kushoto) katika ukaguzi wa Mradi

Kwa upande wake, Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET-SUA, Dkt. Winfred Mbungu, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unafanyika katika kampasi zote tatu za SUA.

Ameeleza kuwa kama sehemu ya timu ya usimamizi, imeendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kila hatua kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kushughulikia changamoto zinazojitokeza huku wakizingatia utunzaji wa mazingira.

Mradi wa HEET ambao unatekelezwa kwa muda wa miaka mitano (2021–2026), unakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 73. Baada ya kukamilika kwake, SUA inatarajia ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi, kuwafikia watu wenye mahitaji maalum na jamii kwa ujumla katika kampasi zake zote.




Post a Comment

0 Comments