SUAMEDIA

Kutoka changamoto hadi faraja: Safari ya mwanafunzi Samson SUA

 

Na: Vumilia Kondo

Samson Laizer, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayesoma Shahada ya Kilimo na Masoko ya Kibenki (Bachelor in Agriculture and Banking) katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ni mfano halisi wa jinsi mazingira jumuishi yanavyoweza kuleta mabadiliko chanya kwa mtu mwenye ulemavu. 


Akiwa na changamoto ya ufupi  ambayo inamzuia kutumia viti vya kawaida darasani, Laizer alikumbana na ugumu mkubwa wa kujifunza.

 Lakini yote hayo yamebadilika, SUA kwa kuzingatia sera yake ya kuwajali watu wenye ulemavu, ilimtengezea kigoda maalum kinachomuwezesha kukaa vizuri darasani na kujifunza kwa utulivu.

“Sikuweza kabisa kutumia kiti cha kawaida, lakini sasa nina kigoda changu maalum. najisikia furaha na amani ninapokuwa darasani,” anasema Laizer huku akitabasamu.

Zaidi ya hapo, suala la usafiri lilikuwa kikwazo kingine kikubwa kwake na wenzake wenye ulemavu.

 


Kutembea kutoka hosteli hadi madarasani ni changamoto, hata hivyo, SUA imehakikisha hakuna anayekatishwa tamaa, bajaji maalum ya Chuo huwachukua na kuwapeleka madarasani kila siku.

“Ni jambo la faraja sana, nimeamua kuja kwa Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda kumshukuru kwa jitihada hizi,” anaongeza Laizer.

Lakini msaada huu si wa bahati mbaya, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Chibunda amesema ni sehemu ya sera ya ndani ya Chuo ya kuwajali wanafunzi na wafanyakazi wenye ulemavu.

Kupitia mradi wa HEET, SUA imeongeza uwezo wake zaidi , ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya teknolojia kusaidia wanafunzi na wafanyakazi wenye changamoto ya uono  kama vile  vishikwambi , mashine za nukta nundu, na vifaa vya kusaidia usikivu kwa wanafunzi na wafanyakazi wenye tatizo la usikivu.

“Tunaendelea kuboresha huduma hizi kwa kadri ya uwezo wetu, na tumepokea ushauri wa Laizer kwa mikono miwili,” amesema Prof. Chibunda.

Kwa Laizer, SUA si tu mahali pa kusoma , ni familia, ni mahali salama pa kutimiza ndoto.

“Naomba kuwashauri wenzangu wenye ulemavu, msikae kimya, msijifiche , njooni SUA hapa mnapokelewa, mnaunganishwa, na mnasaidiwa msikate tamaa,” anahitimisha kwa msisitizo.

 

Post a Comment

0 Comments