SUAMEDIA

Mradi wa CLARITY wabadilisha Usimamizi wa Maji na Maisha Dodoma

 

Na: Mwandishi Wetu

Mradi wa Utafiti wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY) unaendelea kubadilisha maisha ya jamii kupitia mbinu za ubunifu za usimamizi wa maji na tafiti za bathymetri zinazofanywa mkoani Dodoma.


Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Prof. Japhet Kashaigili,  Kiongozi Mkuu wa Mradi kwa upande wa Tanzania amesema kuwa uchunguzi wa bathymetri unaofanyika katika bwawa la Hombolo, Dodoma, unatoa maarifa muhimu kwa matumizi endelevu ya rasilimali za maji ukiwanufaisha moja kwa moja wakulima na wavuvi.

Prof. Kashaigili ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amesema zaidi ya faida za haraka za kilimo, mradi wa CLARITY unashughulikia pia hitaji muhimu la kutambua njia za maji zinazozingatia usawa, uendelevu, na uwezo wa kustahimili mabadiliko ya tabianchi katika maeneo kame ya kitropiki.

“Mradi huu unapanua njia hizi na kuzihusisha katika michakato ya sera pana pamoja na kuziingiza katika jumuiya za kiutendaji”, amesema Prof. Kashaigili.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Kilimo cha Zabibu cha Umwagiliaji Hombolo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Bw. Stanley Mkamilo amesema kwa sasa wakulima wa zabibu 408 na wavuvi 200 wanategemea maji kutoka bwawa hilo ili kuendeleza maisha yao.

Bw. Mkamilo amesema usimamizi bora wa maji utafungua ekari 302 kwa kilimo cha zabibu, mahindi na mbogamboga na kuweka msingi wa ukuaji mkubwa wa kilimo na uhakika wa chakula ambapo kwa sasa kuna ekari 298 za shamba lenye umwagiliaji tayari likifanya kazi.

"Juhudi zaidi itanufaisha mamilioni ya wanajamii, ikiwa ni pamoja na wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, na hata Serikali kupitia ongezeko la mapato ya kodi," alisisitiza Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Umwagiliaji Zabibu Hombolo Bw. Amos Paligana.

Mradi huu unatekelezwa nchini Tanzania, Niger, Nigeria na India, ambapo Nchini Tanzania, unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa kushirikiana na wadau wengine.

Mradi wa CLARITY unafadhiliwa na msaada wa Uingereza kutoka Serikali ya Uingereza na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Maendeleo (IDRC), Ottawa, Kanada, kama sehemu ya mpango wa utafiti wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu (CLARE).



Post a Comment

0 Comments