SUAMEDIA

Wafanyakazi Vyuo Vikuu waaswa kuepuka unyanyapaa kwa wanafunzi wenye ulemavu

 

Na: Hadija Zahoro

Wafanyakazi wa vyuo vikuu nchini wameaswa kuacha vitendo vyovyote vinavyoweza kuashiria unyanyapaa dhidi ya wanafunzi wenye ulemavu, na badala yake kujenga mazingira jumuishi kwa kuwahudumia kwa kutanguliza utu wao na sio kuangalia ulemavu walio nao.

Wito huo umetolewa na Dkt. Sarah Kissanga, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati wa semina ya utoaji elimu kwa wafanyakazi waendeshaji wa  Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Solomon Mahlangu kuhusu namna bora ya kuwahudumia watu wenye ulemavu na mahitaji maalum.

Dkt. Kissanga amesema bado kuna changamoto ya ubaguzi katika utoaji wa huduma vyuoni, jambo ambalo linawanyima haki wanafunzi wenye ulemavu, “tunawahimiza wafanyakazi wawe waelewa na waepuke kutanguliza ulemavu wa mtu, waangalie mahitaji yake kwanza ili kutoa huduma stahiki,” amesisitiza.

Naye Dkt. Lwimiko Salum Sanga kutoka Idara ya Saikolojia na Mitaala, Shule Kuu ya Elimu UDSM, ameeleza kuwa elimu jumuishi ni muhimu kwa kila mwanafunzi, na kwamba shughuli zote za vyuoni zinapaswa kumlenga kila mmoja bila ubaguzi.

“Ni matumaini yetu kuwa washiriki wa semina hii sasa watakuwa na uelewa wa namna ya kuwashirikisha na kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu na changamoto za afya ya akili katika majukumu yao ya kila siku,” amesema Dkt. Sanga.

Kwa upande wake, Raines Jared Obinya Mwandishi Muendesha Ofisi kutoka Ofisi ya Naibu Mshauri wa Wanafunzi, Kampasi ya Solomon Mahlangu  amesema semina hiyo imemfungua macho kuhusu umuhimu wa kujua changamoto wanazopitia baadhi ya wanafunzi.

“Wapo wanafunzi wengi tuliowahi kuwahudumia bila kujua wanapitia hali ngumu, kupitia semina hii, nimejifunza namna bora ya kuwasiliana nao kwa kutumia lugha sahihi na kuepuka viashiria vya unyanyapaa,” amesema Obinya.

Semina hiyo inalenga kuimarisha uelewa wa wafanyakazi wa vyuo kuhusu usawa, ujumuishaji na huduma shirikishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maaalum ili kuboresha mazingira ya elimu kwa wote.



Post a Comment

0 Comments