Na: Hadija Zahoro
Katika kutekeleza azma
ya Serikali ya kudhibiti na kutokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI pamoja
na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (NCDs) mahali pa kazi, Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) kimeandaa semina elekezi kwa waelimisha rika ili kuwajengea
uwezo wa kusaidia wenzao katika maeneo yao ya kazi na masomo.
Semina hiyo imefanyika Mei 31, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE), Kampasi Kuu ya Edward Moringe na kuhudhuriwa na wanafunzi pamoja na watumishi kutoka Idara na Ndaki mbalimbali za Chuo.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa Semina hiyo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael
Chibunda, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Peter Mwakiluma,
amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha maambukizi mapya ya UKIMWI yanapungua
hadi kufikia asilimia sifuri ifikapo mwaka 2030, sambamba na kutokomeza kabisa unyanyapaa
na vifo vinavyotokana na magonjwa hayo.
Amesema SUA ni taasisi ya Serikali na kwamba imeingia katika mpango wa utekelezaji wa kampeni hiyo kuanzia mwaka 2021 hadi 2026 hivyo wapo katika mkakati wa kutimiza azma hiyo ya Serikali.
Ameongeza
kuwa Serikali imewekeza kwa waelimisha rika katika taasisi, hivyo amewataka kuzingatia
yale watakayoyapata katika semina hiyo elekezi kwa sababu wao ndiyo wanaokwenda
kukutana na wenzao wenye changamoto za kiafya
kwa ajili ya kuwa nao karibu na kwenda kuwaelimisha namna gani ya kuishi na
hata kutoa uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi yao.
“Ni
huduma ambazo zipo, kuna watu wenye changamoto hizo ambao wanapata huduma za
aina zote za kimatibabu lakini hata za namna ya kuishi” amesema Bw. Mwakiluma.
Kwa upande wake, Bi. Hekima Titus Maketa, Mratibu wa Masuala ya UKIMWI na NCDs mahali pa kazi ambaye pia ni Afisa Utumishi wa ICE, amesema matarajio yao ni kwamba waelimisha rika hao watafikisha ujumbe katika idara na vitengo vyao sambamba na waelimisha rika wanafunzi kuwafikishia ujumbe wanafunzi wenzao.
Naye Abdulrahmani Ramadhan Jumaa pamoja na Joan Aloyce, wanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Sayansi ya Familia na Watumiaji, wamesema kuwa kupitia semina hiyo wamejifunza umuhimu wa kuhimiza utamaduni wa kupima afya, kufanya mazoezi na kula vyakula vyenye lishe bora.
0 Comments