SUAMEDIA

Wahitimu 794 Watunukiwa Vyeti SUA

 

Na: Hadija Zahoro

Jumla ya wahitimu 794 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kutoka Programu 77 za masomo,  wametunukiwa vyeti vya kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu,  kati ya hao wanaume ni 495 na wanawake 299.

Akitaja takwimu za wahitimu katika Mahafali hayo yaliyofanyika chuoni hapo katika Kampasi ya Edward Moringe, ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda amesema idadi ya wanawake waliohitimu katika Mahafali hayo ya 45 ni 299, ambao ni sawa na asilimia 37.7 ya wahitimu wote.

Prof. Chibunda ameeleza kuwa wahitimu wa Shahada za Kwanza waliostahili kutunukiwa Shahada ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wapo 677, Shahada za Umahiri wakiwa 80 ambapo wanaume ni 53 na wanawake 27.

Ameongeza kuwa wahitimu kutoka Shahada ya Uzamivu wapo 25, yaani wanaume 17 na wanawake wanane (8), huku wahitimu wa Stashahada wakiwa wanane (8) na wahitimu wa Astashahada wako wanne (4).

Aidha, amesema hayo ni Mahafali ya Kwanza tangu Mwenyekiti Mpya wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Andrew William Massawe, ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongoza kwa kipindi cha miaka minne kuanzia tarehe 6 Mei, 2025.

Amesema uteuzi huo ni ishara ya imani kubwa aliyonayo Mhe. Rais kwa Mwenyekiti huyo wa Baraza katika kukiongoza Chuo. Hivyo, kwa niaba ya Menejimenti na Jumuiya nzima ya Chuo cha SUA, ameahidi kushirikiana naye kwa dhati katika kutekeleza majukumu yake ili kuendelea kukiletea Chuo maendeleo makubwa.

‘‘Tunastahili kujipongeza kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi ya nguvu kazi katika Taifa, Viongozi wa Chuo, wanataaluma na wafanyakazi wote wanastahili pongezi kwa kufanya kazi nzuri inayowawezesha kupiga hatua zaidi za mafanikio hapo chuoni mwaka hadi mwaka, ukizingatia kuwa kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo haijawahi kuwa lelemama,” amesema Prof. Chibunda.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Bi. Dorothy Mwanyika, ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Andrew William Massawe, amesema katika kipindi cha kutoka Mahafali ya 44 ambayo yalifanyika tarehe 17 Oktoba, 2024, mambo mengi yamefanyika na Baraza la Chuo limeendelea kusimamia shughuli za Chuo na kupitisha maamuzi mbalimbali ili kuboresha utendaji na ufanisi wa maendeleo ya Chuo.

 Ameyataja mambo hayo kuwa ni kufanya mapitio ya Bajeti ya Chuo ya mwaka 2024/25 na kuidhinisha Makadirio ya Bajeti ya mwaka 2025/26; kupokea na kuidhinisha Taarifa ya Ukaguzi wa Nje wa Hesabu za Chuo za mwaka 2023/24 ambapo Chuo kilipata Hati Safi, kuridhia Sera na Miongozo mbalimbali ya Uendeshaji wa Chuo, ikiwa ni mapitio ya Mpango Mkakati wa Uwekezaji wa Mradi wa HEET kwa mwaka 2021 mpaka 2026, ili kuhakikisha utekelezaji wa maeneo muhimu unakamilika bila kuathiri malengo ya Mradi.






Post a Comment

0 Comments