SUAMEDIA

SUA mmetunza vizuri historia ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini - Rais Mstaafu Thabo Mbeki

 Na: Siwema Malibiche

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki amefanya ziara  maalumu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  kwa kutembelea Kampasi  ya  Solomon Mahlangu kama alama ya uhusiano  kati ya Tanzania na Afrika Kusini  ambao uliasisiwa  na waasisi ya Uhuru wa nchi hizo.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki akipanda mti katika eneo la makaburi ya wapigania uhuru wapinania uhuru wa Afrika Kusini

Ugeni huo kutoka Afrika ya Kusini umepokelewa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye pia ni Waziri Mkuu Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba na viongozi wengine wa Chuo akiwemo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda Mei 22,2025 Mkoani Morogoro ambapo wameeleza kuwa menejmenti ya Chuo itaendelea kuhifadhi miundombinu ambayo imeachwa na wapigania Uhuru wa Afrika ya Kusini  kwa  faida ya vizazi vijavyo.

Akizungumzia mara baada kufika SUA Rais huyo Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki ameupongeza uongozi wa SUA na Mkoa wa Morogoro  kwa kuendelea kutunza  historia ya wapigania uhuru wa Africa ya Kusini  na historia yake huku akitamani  historia hiyo iendelee kurithishwa kwa vizazi vijavyo kwa maslahi ya nchi zote mbili.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye pia ni Waziri Mkuu Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba akiweka mashada kwenye makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini

Rais huyo  Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini  aliambatana na   viongozi mbalimbali wa kiserikali,  wanafunzi kutoka katika Chuo Kikuu cha Africa Kusini  na  waandishi wa habari  ambapo amesisitiza  kuwa  nchi hiyo inatambua kilichowahi kufanywa na mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kipindi cha kupigania uhuru wake.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amemshukuru Rais   huyo Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini  Mhe. Thabo Mbeki kutembelea katika hospitali  iliyokuwa ikitumika kutoa huduma za kiafya kwa wapigania Uhuru wa Africa Kusini na kuongeza kuwa kama menejmenti ya Chuo itaendelea kutunza na  kuhifadhi hospitali hiyo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda akisalimiana na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki wa Afrika Kusini

Aidha, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki ameweka mashada ya maua katika makaburi  na kupanda mti   kando ya makaburi ya wapigania uhuru wa Taifa hilo ikiwa ni ishara ya kuthamini jitihada walizozifanya kwa nchi hiyo na kutunza mazingira.

Katika Kampasi ya Solomon Mahlangu ugeni huo kutoka Afrika ya Kusini umetembelea maeneo mbalimbali waliyokuwa wanayatumia kipindi cha kupigania uhuru   ikiwemo  hospitali na makaburi ya wapigania Uhuru wa Chama cha ANC ambapo wameonesha  heshima  kwa kupanda  mti na kuweka mashada.






Post a Comment

0 Comments